Heche:Hatuwezi kufanya mazungumzo yoyote kama Lissu yupo gerezani

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema mazungumzo kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yalikwama baada ya upande wa pili kushindwa kuwasilisha mapendekezo yao kwa maandishi kama ilivyokuwa imekubaliwa.

Akizungumza katika mahojiano na chombo kimoja cha habari, kiongozi huyo alisema alikuwa miongoni mwa wajumbe wanne walioteuliwa na Chadema kushiriki katika mazungumzo hayo, na kusisitiza kuwa chama hicho kilikuwa tayari kuendelea na majadiliano kwa njia rasmi.

“Nilikuwa kwenye timu ya watu wanne walioteuliwa na chama chetu kwa ajili ya mazungumzo. Tulipofikia hatua ya kuwataka CCM watuletee mambo kwa maandishi, ndipo mazungumzo yakafikia mwisho,” alisema.

Ameeleza kuwa msimamo wa Chadema si kupinga mazungumzo, bali wanataka yafanyike kwa uwazi na uhalali, akisisitiza kuwa chama hakina hofu ya kukaa meza moja na upande wowote.

“Sisi hatuogopi mazungumzo, hakuna mtu tunaogopa kuzungumza naye,” aliongeza.

Hata hivyo, kiongozi huyo aliweka bayana kuwa suala la msingi kwa sasa ni uwepo wa uongozi halali wa chama katika maamuzi hayo, akimtaja mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye yuko gerezani.

“Tumeshasema wazi, mtu anayeweza kuongoza chama hiki kufanya maamuzi yoyote yuko gerezani. Mwachieni Lissu, fungulieni chama,” alisema Heche

Ameongeza kuwa baada ya chama kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake, hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa kiongozi huyo anakuwa huru ili aweze kuongoza mwelekeo wa maamuzi ya chama, ikiwemo mazungumzo yoyote ya kisiasa.

“Akishakuwa nje, yeye ndiye aliyechaguliwa na mkutano mkuu, ndiye atatuongoza kwenye jambo lolote. Bila yeye, wafungwa hawaruhusiwi kufanya majadiliano,” alisisitiza.

Katika mahojiano hayo, Makamu Mwenyekiti huyo pia alikosoa kile alichokiita vitendo vya “ulaghai na uongo” katika mchakato wa mazungumzo, akisema chama chake hakiko tayari kushiriki katika makubaliano yasiyo ya wazi.

“Tunachokataa sisi ni ulaghai na uongo, kutufanya watoto hayo hatukubaliani nayo,” alisema.

Amesisitiza kuwa Chadema iko tayari kwa mazungumzo ya aina yoyote, lakini chini ya uongozi halali na mazingira ya haki na uwazi, akieleza kuwa Lissu anaweza kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la kisiasa nchini.

“Ni mtu mzuri, atatusaidia sana na atasaidia nchi,” alihitimisha.

Kauli hiyo inakuja katika kipindi ambacho Chadema imeanza kurejea katika shughuli za kisiasa kufuatia kuondolewa kwa zuio la mahakama lililokuwa likikizuia chama hicho kufanya shughuli zake kwa miezi kadhaa.