Serikali imesema itarejesha hekta 74,432 kwa wananchi wa Mbarali zilizokuwa eneo la hifadhi ya Taifa ya Ruaha, baada ya hatua ya wananchi kuziomba kushindikana kwa takribani miaka saba.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, akizungumza katika kikao cha pamoja baina Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, wabunge wa Mbarali, uongozi wa CCM wilayani Mbarali na uongozi wa hifadhi za Taifa (TANAPA), alisema lengo ni kutatua migogoro yote ya mipaka sambamba na kufanya zitumike katika shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwa ni pamoja na ufugaji na kilimo.
“Tunataka kumaliza migogoro yote ya mipaka kwa haraka na kuhifadhi rasilimali maeneo hayo na rasilimali za taifa na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema waziri.
Amesema katika kipindi hiki kifupi serikali imefanikiwa kutatua migogoro ya mipaka iliyodumu kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na eneo vijiji vya Tarime vinavyozunguka hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Hata hivyo, Waziri Mchemgerwa alisisitiza na kuwasihi wananchi kutambua umuhimu wa maeneo ya hifadhi yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kusema ndizo vyanzo vya maji yanayokwenda kwenye bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ambalo ndilo chanzo kikuu cha uzalishali wa umeme nchini.