Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Hichi ndicho kilichomponza Luhaga Mpina hadi kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili. - Mwanzo TV

Hichi ndicho kilichomponza Luhaga Mpina hadi kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili.

Jana Juni 18, 2024 Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, alilitangazia bunge na kutoa amri chini ya mamlaka aliyonayo ya kumfikisha mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kutokana na kwamba amelidharau bunge na mamlaka ya Spika.

Hii ni baada tuhuma alizozitoa Mpina dhidi y Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwamb ni za uongo.

Spika amepeleka mbele ya kamati hiyo nyaraka za ushahidi wa Mpina dhidi ya Bashe aliyemtuhumu kwamba amelidanganya Bunge kuhusu utoaji wa vibari vya kuingiza sukari nchini.

Licha ya Spika kuwa na mamlaka ya kutoa adhabu kwa mbunge anayetenda makosa ya kinidhamu, amesema ameamua kumpeleka mbunge huyo kwenye kamati ya maadili kwa kuzingatia utawala bora.

“Mathalani kwa mujibu wa kanuni ya 83, fasili ya pili ya kanuni za kudumu za Bunge, Spika anaweza kumsimamisha mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 10 mfululizo,” amesema Spika.

Amesema kwa kutambua na kuzingatia misingi ya utawala bora, ikiwemo haki ya kusikilizwa amelipekeka suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Kwa upande wa ushahidi uliowasilishwa na Mpina kuthibitisha tuhuma zake kwamba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema uongo bungeni, naikabidhi pia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ushahidi wote ili kamati iupitie na kutoa maoni iwapo ushahidi huo unathibitisha tuhuma kwamba amesema uongo bungeni na nini kifanywe na Bunge,” amesema.

Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Ally Makoa na Makamu Mwenyekiti, Dk Thea Ntara imeanza kazi hiyo Juni 18, 2024.

“Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ianze kuyashughulikia masuala haya mawili leo Juni 18, 2024 na kuwasilisha taarifa kwangu Jumatatu ya Juni 24, 2024. Bunge litashauriwa juu ya maamuzi aliyoyafanya Mpina,” amesema.

Spika amesema Juni 4, 2024, Mpina alitoa taarifa wakati Bashe akichangia kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha kwamba anasema uongo, hivyo alimwelekeza ifikapo Juni 14, 2024 awe amewasilisha ushahidi kwake.

“Hata hivyo, kabla sijachukua hatua yoyote kujiridhisha kuhusu ushahidi huo au kuupeleka kwenye kamati ili kamati ichambue ijiridhishe na kuleta taarifa kwangu.”

“Mpina aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza aliyoyaeleza. 

Kuanzia Juni 14, 2024 baadhi ya vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii imeendelea kurusha mkutano huo wa Mpina na watu mbalimbali wameendelea kuchambua nyaraka zilizowasilishwa kwangu na Mpina na wengine kutoa kabisa hukumu,” amesema Spika.

Amesema Mpina amekuwa bungeni kuanzia mwaka 2005, hivyo ni mbunge mzoefu na anazifahamu ipasavyo sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza Bunge, hivyo ni dhahiri kitendo cha yeye kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwa Spika na wakati huohuo kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya nyaraka hizo ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika

“Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, sura 296 kinazuia kitendo cha kumkosea heshima Spika.”

“Kifungu cha 26 (e) kinazuia vitendo vya dharau kwa mwenendo wa shughuli za Bunge, aidha kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni pasipo kupata kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani,” amesema.

“Kitendo cha Mpina kinakwenda kinyume cha kifungu cha 29 (d na e) na kifungu cha 34, kifungu kidogo cha kwanza (g) vya sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge sura 296.”

“Baada ya kuyatafakari mazingira ambayo suala hili lilijitokeza na alichokifanya Mpina Juni 14, 2024 ni maoni yangu kuwa Mpina amemkosea Spika na vilevile amelikose Bunge,” amesema na kuongeza:

“Hii ni kwa sababu amepoka fursa ya Spika na Bunge kutumia mamlaka waliyopewa kikanuni kufanyia kazi ushahidi alioutoa bila kuendeshwa na mashinikizo kutoka kwa umma ambao unaendelea kujadili ushahidi huo na kutoa hukumu.”

Tuhuma zilipoanzia 

Spika akitoa taarifa chini ya kanuni ya 39, fasili ya pili ya Kanuni za Kudumu za Bunge, amesema Juni 4, 2024, katika kikao cha 40 cha Mkutano wa 15 wakati wa mjadala  wa hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Waziri Bashe alichangia.

Amesema Bashe alichangia  kwamba kampuni na viwanda vya sukari nchini vilivyopewa dhamana na Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na sukari ya kutosha nchini vimeshindwa kutekeleza wajibu huo na kushindwa kuagiza na kusambaza sukari kutoka nje ya nchi kama inavyotakiwa.

Hali hiyo alisema imesababisha kuendelea kuwepo kwa tatizo la uhaba wa sukari nchini.

Spika amesema Bashe alieleza jambo hilo lilisababisha bei ya sukari kuendelea kupanda hadi kufikia Sh10,000 kwa kilo moja.

Amesema wakati Bashe akiendelea kuzungumza Mpina alipata nafasi ya kutoa taarifa kuhusu mchango huo.

“Taarifa ya Luhaga Mpina ililenga kuonyesha Waziri alikuwa analidanganya Bunge kwa sababu kampuni na viwanda vilivyopewa dhamana ya kuagiza sukari havijashindwa kutimiza wajibu wao, bali upande wa Serikali umekuwa ndiyo kikwazao cha kufanikisha lengo hilo.”

“Serikali imeshindwa kushirikiana vyema na wenye viwanda na kampuni zilizopewa dhamana ya kuagiza sukari, hivyo kusababisha kuadimika kwa sukari, kupanda bei, hivyo kuleta kadhia kwa wananchi,” amesema.

“Mpina aliendelea kusisitiza Waziri amelidanganya Bunge na anao ushahidi unaothibitisha jinsi wizara ilivyochangia kuendelea kwa tatizo la uhaba wa sukari nchini,” amesema.

Amesema baada ya taarifa ya Mpina alitoa ufafanuzi kuhusu masharti ya kanuni ya 70 fasili ya kwanza, ya pili na ya tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

“Kanuni inafafaua kuhusu kutosema uongo bungeni, mbunge yeyote anayetoa tuhuma kwamba mbunge mwingine anasema uongo bungeni anatakiwa kuwasilisha ushahidi ili kuthinitisha uongo huo.”

“Hivyo, kwa kutumia kanuni hiyo niliekeza Mpina awasilishe ushahidi ifikapo Juni 14, 2024 ili kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri wa Kilimo amelidanganya Bunge,” amesema.

Spika amesema Juni 14, 2024 Ofisi ya Bunge ilipokea barua kutoka kwa Mpina iliyowasilisha nyaraka za ushahidi kama alivyoelekeza.

Hivi karibuni Mpina amekuwa mwiba kwa wabunge wenzake hasa Mawaziri kutokana na ukosoaji wake mkubwa ambao kimsingi umekuwa ukitafakarisha kutokana na kwamba si jambo la kawaida kwa mbunge wa chama tawala kuikosoa Serikali na Mawaziri wake kama ambavyo yeye amefanya.

Baadhi ya watu wanasema huenda ni mpango mkakati na kwamba  yupo mtu nyuma yake anayemtuma Mpina kufanya hivyo na wengine wanasema huenda ni kwa sababu amekosa teuzi.