Hivi ndivyo Mwanaharakati Maria Sarungi alivyotekwa nchini Kenya

Mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu kutoka  nchini Tanzania Maria Sarungi alitekwa nyara kwenye mitaa ya jiji kuu la Nairobi, Kenya, siku ya Jumapili Januari 12,2025, na aliachiliwa baada ya makundi ya haki za binadamu  kuingilia kati kwa haraka.

 Maria Sarungi Tsehai, ambaye anahamasisha mabadiliko ya kisiasa na haki za wanawake nchini Tanzania, amepata umaarufu mkubwa, akiwa na wafuasi takribani milioni 1.3 kwenye mtandao wa X, lakini amekuwa akiishi uhamishoni katika miaka ya hivi karibuni.

Hii si mara ya kwanza Maria kufatiliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni watekaji ambapo wote waliojaribu kumteka wanahusishwa na mamlaka.

Lakini tukio la kutekwa Maria Sarungi na kisha kujinasua kwa watekaji siku ya Jumapili Januari 12, 2025 lilikuaje?

Shirika la Amnesty International lilitoa tahadhari Jumapili, likisema kwamba alitekwa nyara na wanaume watatu wenye silaha waliokuwa kwenye gari la Toyota Noah la rangi nyeusi ,katika eneo la Kilimani, katikati ya Nairobi.

Eneo hilo inadaiwa kuwa Maria alitekwa akiwa anatoka saluni.

Kwa mujibu wa Mume wake David Tsehai, ni kwamba majira ya saa tisa alasiri mke wake Maria Sarungi alimtumia ujumbe kwamba anatoka saluni anarejea nyumbani, hata hivyo alipoona muda unazidi kwenda na hajafika nyumbani alilazimika kutoka nje ya nyumba na kupewa taarifa na mlinzi kwamba watu watatu walimteka Maria.

“Mchana wa leo (jana) umekuwa mbaya zaidi maishani mwangu, Maria alinitumia ujumbe katika majira ya saa tisa mchana akisema anatoka saluni kurudi nyumbani, lakini ilipofika saa tisa na nusu kwa sababu hakuwa amefika nikaona nitoke nije hapa hapa(saluni), nilivyofika hapa walinzi waliniambia watu watatu wenye silaha walimteka Maria wakati akielekea kwenye Uber” alisema David alipokuwa akizungumza na wanahabari muda mchache tu tangu mke wake alipotekwa nyara.

Shirika lake, la Change Tanzania, lilandika kwenye X kwamba walidhani wahalifu wale ni “maafisa wa usalama wa Tanzania wanaofanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kukabiliana na wakosoaji”

Msemaji wa Amnesty International Kenya, Roland Ebole amesema watu hao watatu waliomteka Maria bado hawajafahamika isipokuwa kwa mujibu wa maelezo ya Maria ya awali aliweza kuwatambua kwa lafudhi zao kwamba watatu ni raia wa Tanzania na mmoja ni Raia wa Kenya na katika mazungumzo yao walimuonya Maria kutokana na ukosoaji wake dhidi ya Serikali ya Tanzania.

Maria Tsehai, mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu, alikimbilia Kenya mwaka 2020, akiomba hifadhi baada ya kukabiliwa na vitisho vilivyoongezeka chini ya serikali ya hayati Rais John Magufuli.

Katika miezi ya hivi karibuni, alielezea wasiwasi wake kwa Amnesty International kuhusu usalama wake, akiripoti tukio ambapo wanaume wawili wasiojulikana walionekana wakimtafuta nyumbani kwake alipokuwa hayupo.

Hii si mara ya kwanza raia wa kigeni kutenkwa nchini Kenya.

Mwezi Novemba mwaka jana mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye alitekwa mjini Nairobi na watu wasiojulikana na kurejeshwa nyumbani kwao Uganda.

Wakimbizi wannne Wa Kituruki pia walitekwa na kutimuliwa kwa lazima hadi Ankara, ambako walikabiliwa na tuhuma za kula njama dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdogan.

Leo Maria anatarajia kuzungumza na wanahabari kueleza namna alivyotekwa hadi kujinasua kwenye mikono ya watekaji