HRW: Kutowajibishwa kwa Polisi nchini Kenya kunaongeza hatari ya vurugu za uchaguzi nchini humo

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo kushindwa kwa mamlaka ya Kenya kuwawajibisha polisi kwa tuhuma za kuua mamia ya watu baada ya uchaguzi wa mwaka 2017, kunaongeza hatari ya polisi kutumia mamlaka yao vibaya kuelekea uchaguzi mkuu wa wiki ijayo. 

Human Rights Watch imesema mamlaka imeshindwa kuchunguza tuhuma za ukatili wa polisi au kufanya mageuzi katika idara hiyo, na kuongeza wasiwasi wa kutokea kwa ghasia iwapo matokeo ya uchaguzi yatapingwa. 

Polisi wa Kenya aghalabu hushtumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kufanya mauaji kinyume cha sheria, hasa katika vitongoji maskini. 
Shirika hilo limeanisha mauaji ya angalau watu 104 wanaodaiwa kuuawa na polisi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, wengi wao wakiwa wafuasi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.