Hukumu ya Sabaya na wenzake yaahirishwa

Hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita sasa itasomwa Juni 10 mwaka huu.

Awali Hukumu hiyo ilikuwa isomwe leo Mei 31, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, lakini imeaairishwa na Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Fadhili Mbelwa kwa maelezo kuwa hakimu Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo yuko nje ya mkoa kikazi. 

‘’Naahirisha kesi hii hadi Juni 10 mwaka huu, kwani Hakimu Kisinda yuko nje ya mkoa kikazi na siku hiyo atakuwa amesharudi,’’ amesema Mbelwa. 

Washitakwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Syliverster Nyegu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Mashitaka matano yanayowakabili washtakiwa hao ni uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuomba rushwa ya Sh milioni 90 na kutumia madaraka vibaya.

Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka jana na kesi yao ilianza kusikilizwa Oktoba, mwaka jana.

Upande wa Jamhuri unaongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Felix Kwetukia akisaidiwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi, Tasila Asenga, Ofmed Mtenga, Neema Mbwana na Richard Jacopiyo ambaye ni Wakili wa Takukuru.

Upande huo ulikuwa na mashahidi 13 na vielelezo tisa na upande wa utetezi ulipeleka mashahidi nane.

Wakili Mosses Mahuna anaongoza jopo la mawakili wa upande wa utetezi akisaidiwa na Faudhia Mustapher, Edmund Ngemela, Fridorini Bwemelo na Sylivester Kahunduka.

https://mwanzotv.com/2022/05/31/mahakama-kuamua-hatma-ya-sabaya-na-wenzake-leo/