Hukumu yaondoa sharti la BAKWATA kwa taasisi za Kiislamu

Baadhi ya waislamu nchini Tanzania wamesema kuwa hawana uongozi wa moja kwa moja chini ya taasisi moja baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kubainisha kuwa serikali haikuwa na mamlaka ya kuwateulia chombo cha kuwaongoza.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, taasisi na mabaraza mbalimbali ya Kiislamu sasa yanaweza kuendesha shughuli zao na kuchagua viongozi wao bila kulazimishwa kuwa chini ya mwamvuli mmoja.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa  tafsiri ya Kiswahili ya hukumu hiyo, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema hapo awali Waislamu walionekana kuwa chini ya chombo kimoja cha uongozi, ambacho ni BAKWATA lakini baada ya uamuzi wa mahakama mambo yamebadilika.

Amesema kwa sasa kuna taasisi na mabaraza tofauti ya Kiislamu yanayoweza kufanya kazi zake kwa uhuru bila kulazimishwa kuwa chini ya taasisi moja, jambo ambalo linarejesha uhuru wa Waislamu kujiamulia masuala yao ya kidini.

Kwa upande wake, msemaji wa Kamati ya Waislamu 12, Juma Hussein Kilaghai, amesema shauri walilofungua mwaka 2024 lililenga kupinga hatua za serikali kulazimisha Waislamu na taasisi zao kuwa chini ya chombo kimoja cha BAKWATA pamoja na vikwazo walivyokuwa wakikumbana navyo wanapotaka kusajili taasisi zao na kupata ulinzi wa kisheria.

Ameeleza kuwa Mahakama Kuu ilibaini kuwa serikali na BAKWATA walishindwa kuthibitisha kuwa BAKWATA iliundwa na Waislamu wenyewe. 

Aidha, mahakama ilieleza kuwa utaratibu uliokuwa unawalazimisha Waislamu kupata utambulisho wa BAKWATA kabla ya kusajiliwa katika mamlaka za serikali ulikuwa kinyume cha Katiba.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Waislamu 12 imeamua kutafsiri hukumu hiyo kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ili wananchi wengi waweze kuielewa kwa urahisi.