Search
Close this search box.
Africa

Idadi ya Wafugaji jamii ya kimasai wanaohama kutoka Ngorongoro yatajwa kuongezeka

16

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Pindi Chana amesema idadi ya jamii ya wafugaji wanaohama kwa hiyari kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera, Wilaya ya  Handeni, mkoani Tanga inaongezeka siku hadi siku, tangu zoezi hilo lilipoanza.

Waziri huyo ameyasema hayo jana alipotembelea kijiji hicho ambacho ujenzi wa makazi kwa ajili ya wafugaji hao wanaohamia unaendelea, huku tayari nyumba 103 zikiwa zimekamilika.

Chana alisema wananchi hao watakapowasili kijijini hapo watahitaji huduma muhimu ikiwamo miundombinu, hospitali, shule, mambo ambayo yote serikali imeyazingatia ili wakazi wa kijiji hicho wote waishi maisha bora.

“Tunashukuru kutokana na wakazi wa hapa kuwa na utayari wa kuwapokea wageni, wale ni Watanzania wenzetu, kule ndani (Hifadhi ya Ngorongoro) kuna miiko, huwezi kufanya biashara, huwezi kupika. Halmashauri tafadhali zile asilimia 10 zisikawie, wananchi hawa watengewe soko, wafanye biashara kwenye magulio, sindano inauma lakini mwisho wa siku unapona.”

“Mwisho wa siku tunataka maisha bora kwa ndugu zetu hawa wanaotoka Ngorongoro ndiyo maana tunataka wakifika wasikae tu wafanye shughuli mbalimbali za uzalishaji mali maisha yanakuwa bora kabisa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima alisema katika kuwahamisha wakazi hao, serikali mkoani humo pia imezingatia uwapo wa shule za kutosha kwa ajili ya familia zitakazohamia.

“Kwa upande wa shule tumeangalia kwamba je, kwa hizi familia zinazokuja na wingi wa watoto zitatosha kwa ajili ya shule ya msingi na sekondari? tukaona tujenge shule shikizi ili mtoto asitembee umbali mrefu.”

Katika ziara hiyo, Waziri Chana alikagua nyumba zaidi ya 100 zinazojegwa na serikali kupitia wataalamu wa NCAA na kueleza kuwa, sambamba na ujenzi wa nyumba hizo,  imepanga kuongeza vyumba vya madarasa 10 vya shule ya sekondari na sita vya shule ya msingi vitakavyokidhi ongezeko la wanafunzi watakaohamia eneo hilo.

Comments are closed

Related Posts