Imeelezwa kuwa idadi ya Watanzania wanaojisaidia vichakani imepungua kutoka asilimia 5.7 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 1.4 Desemba 2021.
Akizungumza leo kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka mitano ya kampeni ya Nyumba ni Choo, Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kwa sasa serikali imefanikiwa kufikia asilimia 72 za kaya za kitanzania zina vyoo bora lakini kutokana na takwimu kujisaidia barabarani bado watu hawajaacha
“Watu kujisaidia nje tumetoka kwenye asilimia 5.7 mwaka 2017 kwa sasa tumefikia 1.4 Desemba mwaka jana. Kwa sasa tumefanikiwa kufikia asilimia 72 za kaya za kitanzania zina vyoo bora lakini kutokana na takwimu kujisaidia barabarani bado watu hawajaacha,” amesema.
Waziri Ummy amesisitiza kuwa baadhi ya Watanzania bado hawana tabia mtazamo kuhusu choo
“Wengi utamkuta amevaa vizuri ana nyumba nzuri lakini nenda chooni kwake…Watanzania wengi hatuthamini choo, panatakiwa pawe pasafi pa kutulia na ikiwezekana iwe sehemu ya kuondoa msongo wa mawazo,”. amesema Waziri Ummy.
Amesema sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu itatoa takwimu halisi ni kwa kiasi gani Watanzania wamefanikiwa katika kuwekeza katika kuwa na vyoo bora, kwani hadi sasa halmashauri zilizoweza kufanya vizuri ni pamoja na Halmashauri ya Njombe ambayo ina asilimia 100, Iringa 86.6 na halmashauri ya Moshi ni asilimia 85.
Mratibu wa Kampeni hiyo Anyitike Mwakitalima amesema awamu ya pili ya kampeni hiyo Serikali imetoa Sh150 bilioni kushughulikia masuala ya maji, vyoo katika shule na maeneo ya mikusanyiko.
“Tumefanikiwa kuongeza idadi ya kaya zinazotumia vyoo bora mwaka 2017 wakati tunaanza kampeni zilikuwa asilimia 37.1 pekee na zenye eneo lakunawa mikono 14.7 lakini sasa tumefikia asilimia 72.1 ya kaya zina vyoo bora na kunawa mikono 41.4 kwa kipindi cha miaka mitano,” amesema Anyitike.
Amesema malengo ifikapo mwaka 2025 asilimia 100 ya kaya ziwe na vyoo bora na zisizo na vyoo zisiwepo kabisa.
Katika hatua nyingine Waziri Ummya amesema kwa sasa Serikali inakwenda kutoa kipaumbele katika usafi wa afya na mazingira kuwa ni uboreshaji wa hali ya vyoo mashuleni utakaohusisha kuongeza matundu na upatikanaji wa maji safi na salama.
Hayo yanakwenda kufikiwa wakati Serikali ikiwa imetoa kiasi cha shilingi bilioni 150 katika awamu ya pili ya kampeni ya Nyumba ni Choo, huku uboreshaji huo ukitazamiwa kufanyika katika shule za msingi na sekondari.
“Eneo tunalokwenda kulipatia kipaumbele ni vyoo shuleni, tuongeze matundu na kujenga vyoo bora, kuna shule unatembelea zina watoto 2000 mpaka 3000 ina matundu matano.
Pia ametaja upatikanaji wa maji kwenye shule nyingi kuwa bado haukidhi mahitaji ya watoto waliopo hivyo bado kunakuwa na changamoto katika masuala ya afya.
“Bado shule zetu hazina maji, lakini pili vyoo vilivyopo ni vichafu awamu hii lazima tuhakikishe shule za msingi na sekondari zinakua na vyoo bora na maji ya kutosha hivyo kupitia awamu hii ya pili tunaendelea kuhakikisha tunaboresha hali ya vyoo mashuleni,” amesema.