IGP Sirro atuma salamu kwa “Vishandu”

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro, ameagiza kufanyika kwa operesheni za kuwasaka na kuwakamata wahalifu wanaotumia pikipiki kupora maarufu kama ‘vishandu’ pamoja na wahalifu wanaojihusisha na uvunjaji na kuiba mali za wananchi.

IGP Sirro amesema hayo wakati alipofanya ukaguzi wa ghafla kwenye kituo cha Polisi Stakishari, Tabata Shule na Kawe Jijini Dar es salaam, ambapo kwenye ukaguzi huo amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Watendaji Kata na Polisi Kata kuendelea kuhamasisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha matukio ya uhalifu yanapungua kwenye maeneo yao.

“Vishandu vimeongezeka mtu ameshika mkoba wake dereva wa bodaboda anatoka nyuma anakuja kupora mkoba, kwa hiyo oparesheni ya  nguvu zifanyike kuhakikisha kwamba haya matukio yanapungua kwa kiasi kikubwa”

Aidha, IGP Sirro amewataka madereva hasa wa pikipiki maarufu bodaboda kufuata masharti ya leseni zao na kuacha kujiingiza kwenye matukio ya uhalifu wa kutumia nguvu.

IGP Sirro amesema kwa sasa matukio ya uhalifu yanaendelea kupungua, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa polisi katika uendelezaji wa kudhibiti matukio ya uhalifu nchini.