Kamati ya Bunge ya Miundombinu imesema matatizo ya kiusanifu ya injini za Airbus A220-300 ambazo zimekuwa zinapata hitilafu mara kwa mara, yanasababisha kukosa mapato wastani wa Sh. bilioni 127.3 kwa mwaka.
Akiwasilisha bungeni jana Januari 4,2025, taarifa ya mwaka ya kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso, alishauri serikali iharakishe upatikanaji injini mbadala za ndege aina ya A220-300 na pia itafute namna bora ya kuhakikisha ndege hizo zinaleta faida kwa nchi.
Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni upatikanaji vipuri kutokana na kushuka kwa uzalishaji vipuri hivyo duniani kutokana na athari za UVIKO-19.
Alisema ATCL pia inakabiliwa na uhaba wa marubani, hususan marubani viongozi, na wahandisi wenye leseni ya kuruhusu ndege kuruka baada ya matengenezo kukamilika.
Kadhalika amesema kuna madeni yanayotokana na mkataba wa ukodishaji ndege kati ya ATCL na TGFA. Deni ya nyuma la TGFA ni Sh. bilioni 429 hadi Juni, 2024 na deni la taasisi za serikali ni Sh. bilioni 64 huku madeni ya wazabuni yakiwa Sh. bilioni 18.
“Serikali ifute deni la TGFA la Sh. bilioni 429, isimamie taasisi nyingine za serikali kulipa Sh. bilioni 64 kwa ATCL na kulipa madeni ya wazabuni Sh. bilioni 18 ili kuondoa changamoto ya madeni ya nyuma yanayolikabili shirika,” alisema.
Amesema serikali iendelee na mchakato wa kuhamisha ndege kutoka TGFA kwenda ATCL na isimamie kuboreshwa sheria ya uanzishwaji ATCL ili itambulike kama kampuni badala ya shirika la umma.