Huku bei ya ngano ikiendela kupanda kutokana na vita nchini Ukraine, waokaji mikate katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast wanaanza kutumia unga wa muhogo unaozalishwa nchini humo kuoka mkate.
Baguette, mkate ambao unapendwa sana katika koloni za zamani za Ufaransa, kwa kawaida huonekana kama kigezo cha gharama ya maisha.
Lakini Ivory Coast haizalishi ngano, badala yake inaagiza kutoka nje hadi tani milioni moja za nafaka kwa mwaka, hasa kutoka Ufaransa.
Kupanda kwa bei ya ngano kumezua wasiwasi kuhusu athari ya uhaba huo katika nchi hiyo ya watu milioni 25 ambapo wastani wa mshahara ni chini ya faranga za CFA 250,000 ($400) kwa mwezi, na ambayo ilitikiswa na wimbi la vurugu katika miaka miwili iliyopita.
Ukraine na Urusi zote ni wazalishaji wakubwa wa ngano, na kutokuwa na uhakika kwa uzalishaji wa nafaka hiyo kumeongeza bei ya bidhaa hiyo.
Waoka mikate, kwa msaada wa serikali, pia wanaanza kubadilisha sehemu ndogo ya unga wa ngano na unga kutoka kwa mihogo.
Muhogo, pia huitwa manioc, ni zao la pili kwa ukubwa nchini Ivory Coast baada ya viazi vikuu, na tani milioni 6.4 huzalishwa kila mwaka.
Lakini watu wa Ivory Coast wanafikiria nini?
“Kila kitu kimekuwa ghali sokoni,” alisema Honorine Kouamee, mchuuzi wa chakula katika wilaya ya Blockhaus ya Abidjan ambaye alikuwa akipika chapati zilizotengenezwa kwa ngano iliyochanganywa na unga wa nazi.
“Kama tunaweza kutengeneza mkate kwa unga wa muhogo wa kienyeji itakuwa bora zaidi. Watu wako tayari kula bidhaa za ndani.”
Shirikisho la taifa la walaji limeunga mkono kwa matumizi ya unga wa muhogo.
“Itatoa kichocheo kwa wazalishaji wa muhogo na kudumisha bei ya mkate,” alisema rais wake, Jean-Baptiste Koffi.
Lakini muonekano wa mkate na ladha ni muhimu na waokaji wengine ni waangalifu.
Mwaka jana, asilimia 10 ya bajeti ya taifa ya karibu dola bilioni 16 ilitumika kuagiza chakula kutoka nje, licha ya kuwepo kwa ardhi yenye rutuba nchini humo.
Wasiwasi katika Afŕika Maghaŕibi kuhusu utegemezi wa ngano kutoka nje hauko nchini Ivoŕy Coast pekee.
Mnamo Julai 19, waokaji mikate kutoka kote Afrika Magharibi watakutana katika mji mkuu wa Senegal Dakar kuzindua chama cha waokaji mikate.
kushawishi kuweka kigezo cha kikanda cha hadi asilimia 15 ya maudhui ya ndani katika bidhaa za mkate.
Kutumia bidhaa za ndani katika kuoka mkate kunaweza ‘kutatua migogoro ya chakula,” alisema Marius Abe Ake, ambaye anaongoza chama cha waokaji.
“Tunahitaji kuoka mikate ya Kiafrika kusaidia kupunguza gharama za utengenezaji, kupambana na umaskini na kuepuka machafuko yanayoharibu.”
Mnamo 2020 watu wengi walikufa katika ghasia za kabla ya uchaguzi — kipindi ambacho kilifufua kumbukumbu za kiwewe za mzozo mfupi wa wenyewe kwa wenyewe mnamo 2011 ambapo maelfu ya watu waliuawa.
Mwaka 2008 ghasia zilizuka wakati gharama ya mchele, maziwa na nyama ilipopanda.