Jaji anayesimamia Kesi ya Mbowe na Wenzake ajitoa

Photo: Jaji Elinaza Luvanda


Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwawakilisha  wenzake watatu leo amemuomba Jaji Elinazer Luvanda ajitoe kusikiliza kesi inayowakabili wakidai kuna taarifa zinazodai hatotenda haki wakati wa usikilizwaji wake kwani ametumika kwa kazi maalum. Mbowe ameyasema hayo leo mara baada ya Jaji anayeendesha kesi inayowakabili kutupilia mbali mapingamizi mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala.

Photo: Freeman Mbowe-Akiingia Mahakamani leo

Mwenyekiti huyo wa CHADEMA anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye makosa ya ugaidi ndani yake, akiwawakilisha wenzake watatu, amesema washtakiwa hawapendezwi na mchakato wa utolewaji wa maamuzi kuhusu mapingamizi yaliyotolewa na mawakili wao. Maamuzi hayo yalitolewa licha ya mawakili wao kutumia vifungu mbalimbali vya sheria ambavyo kimsingi vinaweka wazi mwenendo wa shauri hilo. Moja ya maamuzi uliopingwa na washtakiwa ni Jaji Luvanda kukubali kuwa Hati ya Mashtaka ina mapungufu, lakini alitoa uamuzi kuwa upande wa Jamhuri ukarekebishe hati hiyo, kitu ambacho upande wa mashtaka haukuomba.

Kesi imeahirishwa hadi pale itakapopangiwa Jaji mwingine. Washtakiwa wamerudishwa mahabusu.