Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa Watanzania kubadili mtazamo kwanza badala ya kutaka mabadiliko ya Katiba na Sheria kabla ya kupima vifungu vilivyopo kama vinatekelezeka na kuleta matokeo bora yanayotarajiwa katika ustawi wa nchi.
Prof. Juma alitoa wito huo mara baada ya kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Ningependa kuwaambia Watanzania wenzangu, Sheria za Tanzania siyo mbaya, mtazamo ndiyo mbaya. Sheria hii hii ukiipeleka Marekani itafanyakazi vizuri sana. Pengine badala ya kufikiria kufanya mabadiliko ya sheria, tuanze kufikiria mabadiliko ya nafsi. Nafsi zetu zinaheshimu sheria? Nafsi zetu zinafuata utaratibu? Kwa sababu bila sisi wenyewe kufuata utaratibu, hata tukiwa na sheria nzuri namna gani haitasaidia,” alisema.
Aidha, Jaji Mkuu aliwaomba wananchi wanapotaka mabadiliko ya Katiba na Sheria wahakikishe vifungu vilivyopo hivi sasa wanavitumia ili kujua kama kuna changamoto yoyote katika utekelezaji wake kabla ya kufikiria kwamba pengine kuna vifungu vingine huko nje ambavyo vinaweza kuleta matokeo bora zaidi.
Prof. Juma aliwakumbusha wananchi uwepo wa utaratibu wa kushughulikia nidhamu katika ngazi ya Majaji, Mahakimu, ambapo kuna ushiriki wa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, viongozi wa dini na wote hao hukaa kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa watendaji hao wa Mahakama.
“Ukiangalia sheria inayoendesha shughuli za Mahakama imeunda kamati za maadili. Kuna Kamati za Maadili za Majaji, ambazo zinapokea malalamiko ya kinidhamu dhidi ya Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kwenye suala la nidhamu kuna ushirikishi ambapo wajumbe wanakuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na wajumbe ambao wanatoka miongoni mwa maafisa wa Mahakama katika ngazi za chini, lakini wanakaa kwenye ile kamati ya Majaji inayosimamia maadili.
Alibainisha kuwa kwa bahati mbaya wananchi wengi hawaelewi uwepo wa utaratibu wa kupokea malalamiko dhidi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama Kuu na kuna utaratibu wa kumwomba ajileleze mbele ya kamati hiyo na mapendekezo hupelekwa mbele ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na suala hilo likiwa zito hupelekwa kwenye mamlaka ya uteuzi na kuna ngazi zingine za kufanya kama kuna haja ya kumwondoa Jaji kazini.
“Hivyo, mimi nawaomba wananchi watumie mifumo ya kulalamika masuala ya kinidhamu dhidi ya kiongozi yoyote yule ndani ya Mahakama. Jaji Mkuu ni sehemu ya Mahakama ya Rufani na malalamiko ya kinidhamu yanaweza kuletwa na yakashughulikiwa. Vile vile hatua kama hizo zinaweza kuchukuliwa kwa Jaji mwingine yoyote au Hakimu kwa vile hakuna mtu yoyote yule ambaye yupo juu ya sheria na uzuri mfumo wetu umewakilishwa hadi wilayani na mikoani ambapo huweza kupokea malalamiko na kuyashughulikia,” alisema.
Jaji Mkuu alibainisha pia kuwa Kamati ya Maadili ya Majaji sio kwamba haina mashauri inayosikiliza, ambapo malalamiko yanapoletwa hufanyiwa kazi na ile kamati ambayo Jaji Kiongozi anaiongoza ni kamati ambayo inashughulikia masuala ya kinidhamu dhidi ya watumishi wa Mahakama. Hivyo, aliwaomba wananchi wanapokuwa na malalamiko yanayogusa nidhamu watumie mifumo iliyopo ili kuweze kuipima kama inatosha, na kama haitoshi ifanyiwe marekebisho. “Tusifanye marekebisho bila kupima kama vifiungu vilivyopo vinaweza kufanya kazi,” alisema.
Hivyo alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuapishwa kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Jaji Mkuu alimwelezea Dkt Feleshi jinsi alivyokuwa msaidizi wake muhimu alipokuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye kila asubuhi alikuwa anafuatilia kwenye mfumo wa Mahakama kujua hali ya mashauri inavyokwenda, kuangalia ni mashauri mangani yamesajiliwa kwa njia ya mtandao na mashauri mangapi ambayo hayajapangiwa Majaji na Mahakimu.
“Alikuwa anafuatilia mlundikano wa mashauri. Sisi huku Mahakamani tuna utaratibu, kwa mfano shauri likisajiliwa Mahakama ya Mwanzo linatakiwa liwe limeisha ndani ya miezi sita, katika Mahakama wa Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi, shauri linatakiwa limalizike ndani ya miezi 12 na kwa upande wa Mahakakama Kuu na Mahakama ya Rufani, shauri lazima liishe ndani ya miezi 24. Mimi naamini huko unakokwenda utaleta huo mfumo wa watu kutopata usingizi. Usikubali watu walale kwa sababu usimamizi ni jambo ambalo ni muhimu sana,” alisema.
Jaji Mkuu alimwahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali huyo kuwa Mahakama ya Tanzania itaendeleza huo utaratibu aliouweka wa kufuatilia kwa karibu mienendo ya mashauri na kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi yake kwa wakati na hivyo kupunguza malalamiko kwa wananchi.