
Katika ushahidi wake, Mnyika ametoa ufafanuzi kuhusu maandalizi ya CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, msimamo wa chama kuhusu uchaguzi huo pamoja na kauli ya “No Reform No Election” iliyotumika na chama hicho. Pia amekanusha baadhi ya tafsiri zinazohusisha kauli za viongozi wa CHADEMA na matukio ya vurugu yaliyotokea siku ya uchaguzi.
Mnyika amesema CHADEMA ilikuwa imejiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kwa mujibu wa Katiba, licha ya kile alichokiita mapungufu yaliyokuwepo.
Hata hivyo, amesema chama hicho kilikuwa na msimamo kwamba uchaguzi huo haukuwa huru, wa haki wala halali, na kwamba msimamo huo ulitokana na maazimio ya Kamati Kuu ya chama.
Katika sehemu nyingine ya maswali, Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga, amemuuliza Mnyika kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, ikiwemo vurugu, uchomaji wa vituo vya kura na mali pamoja na madai kwamba matukio hayo yalilenga kuzuia uchaguzi.
Mnyika amekiri kuyasikia baadhi ya matukio hayo, lakini amesema hakukubaliana na hitimisho la Tume ya Jaji Chande kwamba matukio hayo yalilenga kuzuia uchaguzi na yalitokana na kauli za wanasiasa.
Haya ni baadhi ya sehemu ya maswali na majibu kati ya Shahidi na Wakili Katuga
Katuga: Ulisema wewe ndiye uliyeenda kuwakilisha chama kwenda kutoa maoni mbele ya Tume ya Katiba na Sheria?
Mnyika: Sahihi
Katuga: Waambie kama unakumbuka kama moja ya mapendekezo yako ni kutohusishwa katika masuala ya uchunguzi?
Mnyika: Ndio.
Katuga: Waambie Waheshimiwa kama unafahamu au hufahamu kwamba kwenye mapendekezo yako ilipelekea sheria ibadilishwe kuwaondoa Wakurugenzi kwenye masuala ya uchaguzi?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Waambie Waheshimiwa kama mlipata nafasi ya kutoa maoni kwenye Tume ya Katiba na Sheria?
Mnyika: Sikupata nafasi kwa sababu nilizimiwa MIC.
Katuga: Ni majibu yako kwamba huu mkutano wa tarehe 3 Aprili ulikuwa ni mkutano wa ndani ambao haukuwa na Mwenyekiti?
Mnyika: Ni majibu yangu.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji, hiyo mikutano isiyokuwa na Mwenyekiti kama inakuwa na ajenda?
Mnyika: Inategemea na mikutano.
Katuga: Waambie Waheshimiwa kama mkutano wa tarehe 3 Aprili kama ulikuwa na ajenda?
Mnyika: Ulikuwa na mada.
Katuga: Waambie kama huo mkutano ulikuwa wa kichama au ni training?
Mnyika: Ulikuwa wa kichama wa kuwaelimisha watia nia.
Katuga: Waambie Waheshimiwa tofauti ya ajenda na mada?
Mnyika: Mada ni jambo linalozungumzwa.
Katuga: Hiyo tafsiri ya ajenda ni kwa mujibu wa ufahamu wako au?
Mnyika: Nimejibu kwa tafsiri yangu.
Katuga: Nitakuwa sahihi kwamba kwa kuwa hakukuwa na mada maalum basi kiongozi alikuwa na nafasi ya kuzungumza chochote alichokifikiria?
Mnyika: Hapana, mkutano ulikuwa na mada.
Katuga: Sasa kama nilikusikia na kukuelewa vyema kwenye neno uasi ukasema ukisema neno uasi si kosa?
Mnyika: Sahihi.
Katuga: Ni kweli au si kweli kwamba tafsiri yako ya neno uasi inatokana na kauli ya Mwalimu Nyerere?
Mnyika: ….
Katuga: Kwa uelewa wako wa kisiasa waambie maana ya neno uasi?
Mnyika: Ni kupinga au kukataa kwa nguvu kubwa sana.
Katuga: Kuhamasisha uasi kupinga uchaguzi maana yake nini?
Mnyika: Ni kukataa au kupinga uchaguzi kwa njia halali za kidemokrasia.
Katuga: Hiyo tafsiri ya uasi uliyoitoa ni kwa mujibu wa kamusi au uelewa wako wa kisiasa?
Mnyika: Uelewa wangu wa kisiasa.
Katuga: Mwaka jana chama chako kilishiriki uchaguzi mkuu?
Mnyika: Hakijashiriki.
Katuga: Kama unakumbuka kwenye hotuba ya Mwenyekiti, je ni kweli aliwaambia watia nia kwamba, “kama unategemea kuwa mbunge mwaka huu sahau”?
Mnyika: Aliwaambia.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama unakumbuka kwamba Mwenyekiti aliwaambia watia nia kwamba na mimi nilitaka nigombee cheo fulani lakini nimesahau?
Mnyika: Hilo neno nimesahau, sikumbuki.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama mlijiandaa kushiriki uchaguzi Mkuu?
Mnyika: Tulijiandaa vizuri.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama mlijiandaa kushiriki uchaguzi wa 2025?
Mnyika: Tulijiandaa kwa mujibu wa Katiba pamoja na mapungufu yake.
Katuga: Waambie kama nimekusikia vizuri unasema kwenye hotuba yake Mwenyekiti alisema tutazuia uchaguzi kwa njia za kidemokrasia?
Mnyika: Sahihi.
Katuga: Waambie kama kwenye ushahidi wako ulisema Mwenyekiti tutazuia uchaguzi kwa njia za kidemokrasia?
Mnyika: Sikusema moja kwa moja.
Katuga: Katika ushahidi wako kama kuna sehemu uliwaambia Waheshimiwa Majaji kwamba njia za kuzuia uchaguzi alizozisema Mwenyekiti ni njia moja, mbili, tatu, ulizitaja hizo njia alizosema?
Mnyika: Niliwaambia.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama kuhamasisha uasi ni njia ya kidemokrasia?
Mnyika: Njia ya kidemokrasia.
Katuga: Waambie kama kuzuia uchaguzi kwa njia ya uasi ni njia ya kidemokrasia?
Mnyika: Ni njia ya kidemokrasia.
Katuga: Umekubali kwamba vyama vingine vina haki ya kushiriki uchaguzi mkuu?
Mnyika: Uchaguzi Mkuu huru, haki na halali.
Katuga: Ule uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa ni uchaguzi wa aina gani?
Mnyika: Haukuwa uchaguzi huru, halali na haki.
Katuga: Je, kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA inaruhusu mtu kuamini anachoamini?
Mnyika: Inaruhusu.
Katuga: Je, Katiba ya CHADEMA inaelekeza mtu asiamini anachoamini ili mradi asivunje sheria?
Mnyika: Inaelekeza.
Katuga: Je, Mwenyekiti katika hotuba yake, kauli yake aliyosema tutavuruga uchaguzi, tutakinukisha, tutahamasisha uasi alilenga kuhamasisha kufanyike mabadiliko ambayo mliyoamini nyinyi kwamba ndiyo yatakayofaa?
Mnyika: Ni kweli.
Katuga: Hivi baada ya Mwenyekiti kuwa amepata kesi hii, ni nani aliyeendeleza hiyo hamasa ya No Reform No Election?
Mnyika: Viongozi wa Kamati Kuu ya Chama akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama, John Heche.
Katuga: Ulikuwa unamuandalia hotuba?
Mnyika: Hapana.
Katuga: Ni kweli kwamba huyu John Heche katika kuendeleza nia aliweza kuongea na EAST Africa Radio kuhusiana na nia hiyo ya kuzuia uchaguzi?
Mnyika: Sijui.
Katuga: Waambie kama unajua kwamba kupitia hiyo redio alitangaza kwamba huo uchaguzi wa 2025 hautakuwepo?
Mnyika: Sijui.
Katuga: Waambie kama unajua au hujui kwamba katika uchaguzi wa mwaka jana kulikuwa na jaribio la kuzuia uchaguzi wa mwaka jana kwa kuchoma vituo vya kura?
Mnyika: Sijui.
Katuga: Waambie kama tarehe 29 Oktoba mwaka jana ulikuwa nchini au hukuwa nchini?
Mnyika: Nilikuwa nchini.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama wewe binafsi ulijitokeza kupiga kura au hukujitokeza?
Mnyika: Sikujitokeza.
Katuga: Kwa msimamo wetu mwaka jana hakukuwa na uchaguzi?
Mnyika: Hakukuwa na uchaguzi.
Katuga: Kwa imani yako ile nia ya kuzuia uchaguzi ilidhihirika?
Mnyika: Sio sahihi.
Katuga: Unajua kwamba katika uchaguzi ule kulikuwa na mali za watu zilichomwa?
Mnyika: Sijui, nilisikia.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji ni sahihi au sio sahihi kwa umma walivyotafsiri wao yale maneno aliyosema Mwenyekiti wako katika hotuba yake ya Aprili 3?
Mnyika: Ni haki.
Katuga: Kwa tafsiri hiyo hiyo kwamba ni haki, nitakuwa sahihi kwamba ni haki kwa umma kuchocheka kuchoma vituo vya kura, kupiga watu, kukata vidole?
Mnyika: Sio haki.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama tarehe 3 Aprili 2025 Mwenyekiti aliwaambia umma, ni lini wazuie huo uchaguzi?
Mnyika: Hakuwaambia.
Katuga: Kwa kuwa hakuwaambia, ni haki au sio haki watu kutoka umma kuzuia uchaguzi siku ya uchaguzi?
Mnyika: Sio haki.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama umesikia Mheshimiwa Jaji Chande akisema kwamba matukio ya Oktoba 29 yalilenga kuzuia uchaguzi?
Mnyika: Nimemsikia lakini hatukukubaliana naye.
Katuga: Waambie kama ulisikia Mheshimiwa Chande alisema matukio yale yalitokana na kauli za wanasiasa?
Mnyika: Tulimsikia lakini hatujakubaliana naye.
Katuga: Ni kweli uliwahi kuwa mbunge?
Mnyika: Kweli.
Katuga: Mbunge wa kuteuliwa au kuchaguliwa?
Mnyika: Kuchaguliwa.
Katuga: Kupitia experience ya ubunge utakuwa unaelewa kidogo wa masuala ya sheria?
Mnyika: Kidogo.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama unafahamu au hufahamu kwamba Tanzania kuwa huru ina Katiba yake?
Mnyika: Ina Katiba yake.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama unafahamu Tanzania kuwa huru kwamba Mahakama ni chombo cha mwisho kuamua kwamba mtu huyu yupo huru au ana hatia?
Mnyika: Mahakama za Tanzania na Mahakama za Kimataifa.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kwamba ushahidi huu unamweka mshtakiwa hatiani au haumtii hatiani?
Mnyika: Sahihi.
Katuga: Kwa uelewa wako DPP akifuta kesi anaweza kuirudisha au hawezi?
Mnyika: Anaweza.
Katuga: Waambie kama unaijua mihimili ya dola?
Mnyika: Naijua.
Katuga: Iko mingapi?
Mnyika: Mitatu.
Katuga: Je, unafahamu kwamba ni Bunge lenye kazi ya kutunga sheria?
Mnyika: Ni kazi moja wapo.
Katuga: Unajua kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria?
Mnyika: Ni moja wapo.
Katuga: Ni kweli kazi ya Serikali ni kusimamia sheria?
Mnyika: Ni jukumu moja wapo.
Katuga: Mtu anapotishia kuvunja amani unakuwa umemtishia Rais na vyombo vyake?
Mnyika: Sio kweli.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji siku ya uchaguzi wa tarehe 29, 2025 amani ilikuwepo au ilitoweka kwa muda?
Mnyika: Kulikuwa na vurugu na kulikuwa na amani.
Katuga: Kama Katibu Mkuu waambie kama kuchoma miundombinu, kuchoma vituo vya kura, waambie kama ni uvunjifu wa amani?
Mnyika: Sifahamu.
Katuga: Katika ushahidi wako ulisema mlipokamatwa kule Mbeya wewe, SUGU na Mwenyekiti wako ulisema Mwenyekiti wako alipelekwa kusikojulikana. Sasa usipopajua wewe au ndiyo huko kusikojulikana?
Mnyika: Nisipopajua mimi.
Katuga: Ni kweli au si kweli kwamba Mbowe alishtakiwa kwa ugaidi?
Mnyika: Kweli.
Katuga: Ni kweli kwamba kwenye kesi hiyo Mbowe alishtakiwa na wengine?
Mnyika: Kweli na mashtaka yao yakafutwa.
Katuga: Ni kweli kwamba hao walioshtakiwa na Mbowe walikuwa ni makomandoo wa Jeshi la Tanzania?
Mnyika: Hilo nilisikia Mahakamani.
Katuga: Kwa kuwa ulisema Mbowe ameshtakiwa kwa sababu ya madai ya Katiba Mpya. Sasa swali ni je, kweli wale walioshtakiwa nao hawakuwa wanaharakati?
Mnyika: Hawakuwa wanaharakati, walikuwa walinzi.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji ulisema wewe ulikuwa afisa masuhuli?
Mnyika: Ndio.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama ulikuwa unahusika kuwalipa hawa walinzi wa Mbowe?
Mnyika: Sikua nahusika.
Katuga: Waeleze kama ulikuwa unatembea nao, unalala nao kuweza kujua yote?
Mnyika: Sikua natembea nao kujua yote.
Katuga: Kwa kuwa hukuwa unatembea nao hujui wanachofanya, nitakuwa sahihi nikisema hujui walichokuwa wanatumiwa nacho?
Mnyika: Najua kilichozungumzwa Mahakamani.
Katuga: Nimekusikia hapa ukisema kwamba kwa ufahamu wako hii kesi ni mwendelezo wa ukandamizaji wa Serikali na vyombo vyake kubambikiza viongozi wa CHADEMA?
Mnyika: Sahihi.
Katuga: Ukisema na vyombo vyake unamaanisha?
Mnyika: Jeshi la Polisi.
Katuga: Ni kosa gani la Jeshi la Polisi kumkamata mtu anayepanga kuvunja usalama wa raia na mali zake?
Mnyika: Sio kosa.
Katuga: Sasa ni sheria gani inayompa Mwenyekiti wa CHADEMA kinga ya kutoshtakiwa na Jeshi la Polisi kama atakuwa na makosa?
Mnyika: Hakuna.
Katuga: Hebu waambie Waheshimiwa Majaji kwamba ulisema baada ya ile kauli ya Mwenyekiti ya tarehe 3 Aprili 2025, Msajili aliwaandikia barua alitaka mjieleze, huo ndio ulikuwa ushahidi wako?
Katuga: Aliwataka mjieleze nini?
Mnyika: Alimtuhumu Mwenyekiti kwa kauli za kisiasa.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama huyu Msajili wa Vyama vya Siasa ana mahusiano na Jeshi la Polisi?
Mnyika: Sio sehemu ya Jeshi la Polisi.
Katuga: Pia nimekusikia ukisema CHADEMA ilizuiwa kushiriki uchaguzi kwa sababu Katibu Mkuu hakusaini fomu za maadili ya uchaguzi?
Mnyika: Sahihi.
Katuga: Uli-saini au hukusaini?
Mnyika: Sikuisaini.
Katuga: Je, sheria inakutaka usaini au usisaini?
Mnyika: Sheria kabla ya uchaguzi ilikuwa hailazimishi.
Katuga: Unajua haki ya kushiriki uchaguzi ni haki ya kikatiba?
Mnyika: Najua.
Katuga: Unajua kwamba kunyimwa kutokushiriki ni kwamba ni haki ya kikatiba?
Mnyika: Ni haki ya kikatiba.
Katuga: Kama mtendaji unajua kwamba kuvunjwa kwa hiyo haki ya kikatiba sheria inaruhusu kuidai hiyo haki ya kikatiba Mahakamani?
Mnyika: Sio haki zote ni lazima uende ukazidai Mahakamani.
Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama chama chako kilizuiwa kushiriki uchaguzi Mkuu na kama kilifungua kesi kuhusu CHADEMA kuzuiwa kushiriki uchaguzi?
Mnyika: Kama chama hakijafungua, ila nafahamu kuwa kuna watu nje ya chama walifungua.
Katuga: Kwa ushahidi wako kuhusiana na masuala ya uchaguzi uliiambia Mahakama kwamba?
Mnyika: Sio huru, sio halali, sio wa haki.
Katuga: Hayo yalikuwa maoni yako au Mwenyekiti wako au wanachama wako?
Mnyika: Ni msimamo wa Chama kupitia maazimio ya Kamati Kuu.
Katuga: Iambie Mahakama hii nitakuwa sahihi nikisema kwamba msimamo wa Mwenyekiti na wewe na wa Kamati Kuu kwamba Tanzania haina uchaguzi huru, sasa njia ya kutumia ni njia isiyo ya kidemokrasia kupata uchaguzi huru?
Mnyika: Sio sahihi.
Kesi inaendelea