Shahidi wa tatu wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, Amani Golugwa, ameendelea kuhojiwa na upande wa mashtaka katika hatua ya pili ya ushahidi wake, huku maswali yakijikita katika mada mbalimbali alizozieleza mahakamani.

Golugwa, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, amehojiwa kuhusu ushiriki wake katika chaguzi mbalimbali, malalamiko ya uchaguzi pamoja na ripoti za waangalizi wa kimataifa wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 alizozitumia kama rejea katika ushahidi wake. Amesema hakugombea nafasi yoyote katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 wala hakujaza fomu za kugombea, lakini alishiriki katika usimamizi wa wagombea wa chama.
Katika mahojiano hayo, Golugwa amesema malalamiko mbalimbali yaliyohusiana na uchaguzi yaliwasilishwa katika Kamati za Rufaa, lakini hakumbuki idadi ya malalamiko ambayo mahakama ziliwahi kuyaona kuwa na mashiko. Amesema baadhi ya taarifa alizozitoa kuhusu wagombea alizipata kutokana na ushiriki wake wa moja kwa moja na wagombea hao.
Pia amekiri kuwa Chadema haikushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akieleza kuwa chama hicho kilizuiwa kushiriki.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo kuzuiwa kushiriki na kuamua kutoshiriki ni jambo moja, amesema mambo hayo mawili hayafanani. Kuhusu madai ya ushirikiano kati ya baadhi ya maafisa wa Tume ya Uchaguzi na CCM katika kuharibu uchaguzi, Golugwa amesema aliwahi kutoa kauli hiyo na kwamba alikuwa katika mazingira yaliyohusishwa na kauli hiyo.
Sehemu nyingine ya mahojiano imejikita katika ripoti za waangalizi wa uchaguzi za mwaka 2025 ambazo Golugwa alizirejea katika ushahidi wake.
Amesema si mwandishi wala mhifadhi wa ripoti hizo na kwamba hakuzileta mahakamani. Ripoti hizo zimeandikwa kwa Kiingereza, huku yeye akizieleza kwa Kiswahili. Alipoulizwa kuhusu uwezo wake wa kufuatilia ripoti ya uchaguzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema hakuiweza kuifuatilia.
Golugwa pia ameulizwa kuhusu uelewa wake wa masuala ya sheria, akisema hana elimu ya sheria. Hata hivyo, amesema anaelewa kuwa maswali ya dodoso ni sehemu ya mchakato wa kisheria na kwamba ushahidi katika kesi ya jinai unapaswa kuzingatia ushahidi badala ya ushabiki wa kisiasa.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka na baadaye Wakili Nasoro Katuga wamechunguza nafasi ya Golugwa ndani ya Chadema.
Golugwa amethibitisha kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu tangu Januari 22, 2023 na kwamba aliwahi kutangaza maazimio ya Kamati Kuu yaliyokuwa katika uwanja wa taarifa za wazi, ikiwemo suala linalohusiana na kesi hiyo.
Kuhusu uteuzi wake kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Golugwa amesema aliteuliwa na Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu.
Kauli hiyo iliibua hoja ya kisheria kuhusu utaratibu wa uteuzi wa viongozi ndani ya chama, ambapo Golugwa amesema iwapo shahidi mwingine angesema Katibu Mkuu anateuliwa na Kamati Kuu, kauli hiyo isingekuwa sahihi kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa.
Golugwa pia amesema amefanya kazi za uhasibu tangu mwaka 2001 na kwamba amekuwa mwandishi wa kumbukumbu za vikao.
Akieleza kuhusu Katiba ya Chadema, amesema kuna aina mbili za vikao, ambavyo ni vikao vya uchaguzi na vikao vya utendaji, huku akikubali kuwa maneno kama “vikao vya ndani” na “vikao vya hadhara” yanaweza pia kutumika kuelezea aina hizo za vikao.
Wakati akiwa Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Golugwa amesema aliandaa taarifa zilizohusiana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Pia amekiri kuwa katika taarifa hizo kulikuwa na msimamo wa Chadema wa kutoshiriki uchaguzi hadi Serikali itakaposhinikizwa kufanya mabadiliko. Alipoulizwa ni nani aliyepaswa kushinikizwa, alijibu kuwa ni Serikali.
Katika mahojiano hayo, Golugwa pia ameeleza kuwa aliwahi kukamatwa mara mbili bila kufunguliwa hati ya mashtaka na kwamba katika matukio yote mawili aliachiliwa baada ya maelezo yake kusikilizwa.
Kesi hiyo ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu inasikilizwa na Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru pamoja na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kuwa Aprili 3, 2025 alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika ushahidi wake wa awali, Golugwa alieleza kasoro alizodai kuwepo katika chaguzi mbalimbali kuanzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitumia ripoti za waangalizi wa kimataifa kama sehemu ya rejea zake.
Pia alikanusha kuwa kauli za Lissu zilizotajwa na upande wa mashtaka zilikuwa na maana ya kutenda kosa la uhaini.
Kesi inaendelea