Jane Goodall: Mwanamke aliyewapa Sokwe sauti na kuigusa dunia

Mwanasayansi maarufu na mwanaharakati wa kimataifa wa mazingira, Dr. Jane Goodall, ambaye aligeuza mapenzi yake ya utotoni kwa sokwe kuwa safari ya maisha ya kulinda mazingira, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91. Taasisi aliyoianzisha imethibitisha kifo chake Jumatano, ikisema alifariki kutokana na sababu za asili akiwa katika  jimbo la California, Marekani, wakati wa ziara ya mihadhara.

Goodall, aliyebobea katika utafiti wa sokwe pori na baadaye kuwa mwanaharakati wa mazingira, alibadilisha mapenzi yake ya wanyamapori kuwa kampeni ya maisha yote. Safari yake ilimtoa kutoka kijiji cha pwani kusini mwa Uingereza hadi Afrika, na hatimaye kumzungusha duniani kote akijitahidi kuelewa sokwe na nafasi ya binadamu katika kulinda makazi yao pamoja na afya ya sayari kwa ujumla.

Katika miaka ya 1960, Goodall alikuwa kinara katika utafiti wa sokwe na mmoja wa wanawake wachache sana waliokuwa wakifanya kazi ya kisayansi ya aina hiyo. 

Alifungua njia kwa wanasayansi wanawake wengine kama marehemu Dian Fossey. Kupitia ushirikiano wake na National Geographic Society, alileta maisha ya sokwe karibu na jamii kwa filamu, runinga na majarida, na kufanya kazi yake ijulikane ulimwenguni.

Goodall alivunja desturi za kisayansi za wakati huo kwa kuwapa sokwe majina badala ya namba, kuonyesha tabia zao binafsi na mahusiano ya kifamilia, na kuchunguza hisia zao. Pia aligundua kwamba sokwe, kama wanadamu, hutumia zana. “Tumegundua kwamba hakuna mpaka mkali kati ya binadamu na wanyama wengine,” alisema katika hotuba yake ya TED mwaka 2002.

Kadri taaluma yake ilivyokua, alipanua utafiti kutoka sokwe hadi kwenye harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi baada ya kushuhudia uharibifu mkubwa wa makazi ya wanyama. Mara kwa mara aliitaka dunia kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo. “Tumesahau kwamba sisi ni sehemu ya ulimwengu wa asili,” aliiambia CNN mwaka 2020.

Kwa mchango wake mkubwa, alipewa heshima nyingi, ikiwemo kuteuliwa kuwa Dame wa Uingereza mwaka 2003, na mwaka huu 2025 alitunukiwa Medali ya Uhuru ya Rais wa Marekani (Presidential Medal of Freedom).

Goodall alizaliwa London mwaka 1934 na kukulia Bournemouth, kusini mwa Uingereza. Ndoto yake ya kuishi na wanyama ilianza mapema akiwa binti mdogo, ilichochewa na zawadi ya nyani wa kuchezea aliyopewa na baba yake, pamoja na vitabu kama Tarzan na Dr. Dolittle.

 Baada ya kumaliza shule, hakupata nafasi ya kwenda chuo kikuu kutokana na hali ya kifedha. Alifanya kazi ya ukatibu na kwenye kampuni ya filamu kabla ya rafiki yake kumualika Kenya, jambo lililompeleka barani Afrika mwaka 1957 kwa kutumia meli.

Safari yake ilianza rasmi alipokutana na mwanakiolojia maarufu Dr. Louis Leakey na mkewe Mary. Chini ya usimamizi wa Leakey, Goodall alianzisha kituo cha utafiti cha sokwe katika Hifadhi ya Gombe, karibu na Ziwa Tanganyika, nchini Tanzania. 

Hapo alibaini sokwe hula nyama, hupigana vita vya kikundi, na muhimu zaidi hutengeneza zana ili kuvua mchwa – ugunduzi uliomfanya Leakey kusema: “Sasa lazima tueleze upya maana ya zana, tueleze upya maana ya binadamu, au tukubali kwamba sokwe pia ni binadamu.”

Ingawa baadaye alisoma shahada ya udaktari wa falsafa (PhD) katika Chuo Kikuu cha Cambridge, aliendelea kurudi Gombe kwa miaka mingi. Mume wake wa kwanza alikuwa mpiga picha wa wanyama pori Hugo van Lawick, ambaye naye alishirikiana naye katika kazi yake. 

Kupitia kazi za National Geographic, sokwe wa Gombe walijulikana duniani kote – akiwemo maarufu David Greybeard, sokwe aliyempa jina kutokana na nywele zake za kijivu.

Baada ya miongo mitatu barani Afrika, Goodall aligundua kwamba sokwe hawawezi kulindwa bila kushughulikia tishio kubwa zaidi – kutoweka kwa makazi yao. Aliona haja ya kuondoka msituni na kuwa mwanaharakati wa kimataifa. Mnamo 1977 alianzisha Jane Goodall Institute, shirika lisilo la kiserikali linalolinda sokwe, mazingira na kutoa elimu ya uhifadhi. 

Baadaye alipanua shughuli zake kupitia mpango wa vijana Roots & Shoots, unaolenga watoto na vijana kushiriki moja kwa moja katika kulinda mazingira.

Katika maisha yake, Goodall alisafiri zaidi ya siku 300 kwa mwaka akizunguka dunia kuzungumza na viongozi wa serikali, mashule na jamii, akihimiza mshikamano wa kulinda sayari. Wiki moja kabla ya kifo chake, bado alikuwa akihutubia mkutano wa hali ya hewa jijini New York.

Mbali na kazi za utafiti na harakati, alikuwa mwandishi mahiri wa zaidi ya vitabu 30, vikiwemo Reason for Hope: A Spiritual Journey (1999) na vitabu kadhaa vya watoto. Alipenda kusisitiza kwamba bado kuna matumaini, akisema: “Ndiyo, kuna tumaini. Iko mikononi mwetu – mikononi mwako, yangu na ya watoto wetu.”

Katika maisha yake ya binafsi, Goodall alipata mtoto mmoja aitwaye Grub na mume wake wa kwanza Hugo van Lawick, kabla ya kuachana mwaka 1974. Mume wake wa pili, Derek Bryceson, alifariki mwaka 1980.

Urithi wake unabaki hai kupitia taasisi alizoanzisha, mamilioni ya vijana aliowahamasisha, na fikra alizobadilisha kuhusu uhusiano kati ya binadamu na wanyama.