Uwepo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Aikaeli Mbowe, katika hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 jijini Dodoma, umeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wake wa kisiasa. Hafla hiyo, iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, huku sura ya Mbowe ikiibua maswali mengi kuhusu nafasi yake ya sasa ndani ya upinzani na mwelekeo wake wa baadaye.
Ukimya wa Mbowe na Mwelekeo Usiojulikana
Tangu alipopoteza nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama hicho mwaka 2025 Januari 22, Mbowe amekuwa kimya hadharani, hali ambayo ni tofauti na mtindo wake wa awali wa kuwa mstari wa mbele katika mijadala ya kisiasa. Wakati wengi walitarajia angerejea katika ulingo wa kisiasa kwa mtindo mpya, Mbowe amebaki kivuli cha kile kilichowahi kuwa sauti kali ya upinzani Tanzania.
Kutoonekana Katika Vikao na Kesi ya Lissu
Kikatiba, Mbowe bado ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, chombo cha juu zaidi cha maamuzi ya chama hicho. Hata hivyo, taarifa zinaonesha kuwa hajawahi kuhudhuria hata kikao kimoja cha Kamati hiyo tangu uchaguzi wa uongozi huo kumalizika na safu mpya ya uongozi kuanza kufanya kazi za Kichama.
Zaidi ya hayo, katika kipindi chote cha mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu aliyekuwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa, Mbowe hakuwahi kufika mahakamani, jambo lililowashangaza wengi, hasa ukizingatia uhusiano wao wa muda mrefu ndani ya CHADEMA.
Tetesi za kuhama chama na uwepo wa wafuasi wake CHAUMA
Duru mbalimbali za kisiasa zimeanza kuibua dhana kuwa Mbowe huenda yuko mbioni kuhamia chama kingine, hasa CHAUMA, ambacho hivi sasa kinaonekana kukusanya baadhi ya waliokuwa wafuasi wake wa karibu ndani ya CHADEMA.
Wengine wanasema, hali ya kutoridhishwa na mwelekeo wa sasa wa CHADEMA inaweza kuwa imemfanya kutafuta jukwaa jipya la kisiasa, ingawa hakuna tamko rasmi kutoka kwake kuhusiana na suala hilo.
Uwepo wake katika hafla ya Serikali: Ishara ya kujiunga na CCM?
Mjadala umechochewa zaidi na picha ya Mbowe akiwa bega kwa bega na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kitaifa ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya 2050, jambo linalotazamwa na baadhi ya wachambuzi kama dalili ya kusogea kwake karibu na serikali au hata Chama cha Mapinduzi (CCM). Hili linaibua swali gumu: Je, Mbowe anajiandaa kwa hatua ya kushangaza ya kisiasa kama vile kujiunga na chama tawala? Swali hili limebaki fumbo ila wakati huenda ukaamua hatma ya Mbowe
Maana na athari kwa siasa za upinzani
Iwapo tetesi hizi zitathibitika kuwa kweli, basi hatua hiyo ya Mbowe inaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa za upinzani nchini. Kama mmoja wa wanasiasa waliowahi kuwa alama ya ukakamavu na uimara wa CHADEMA, uhamaji wake (au hata kimya chake) unaweza kutafsiriwa kama dalili ya mabadiliko ya mwelekeo wa upinzani, kutoka uanaharakati mkali hadi mbinu za kisiasa za maridhiano au hata kujiondoa kwenye ulingo wa siasa kali.
Kwa sasa, Freeman Mbowe bado hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu nafasi yake kisiasa au hatma yake ndani ya CHADEMA. Hata hivyo, mazingira yanayoendelea kujitokeza ikiwamo ukimya wake wa muda mrefu, kutohudhuria vikao muhimu vya chama, kutoshiriki katika kesi ya Lissu, na kisha kuonekana kwake katika hafla ya serikali yote yanachora taswira mpya isiyokuwa na majibu ya moja kwa moja.
Swali kuu linabaki: Je, Mbowe anaandika ukurasa mpya wa kisiasa, au anaufunga kabisa?