Machi 17,2021 Taifa la Tanzania lilikuwa katika simanzi kubwa iliyogubikwa na sintofahamu baada ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo John Magufuli.
Hakukuwa na taarifa za awali juu ya ugonjwa wake kiasi Watanzania wengi waliamini Rais anaendelea na majukumu yake, lakini ilikuwa kinyume kutokana na kiongozi huyo wa nchi kuwa mahututi hospitalini akipambania uhai wake.
Siku hiyo majira ya saa tano usiku, aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo ambaye sasa ni Rais Samia Suluhu, alitangaza kifo cha hayati Magufuli.
Mengi yalisemwa kuhusu kifo hicho huku kukiwa na maoni kinzani, ambapo wapo waliokuwa wanailaumu Serikali kwa kutoweka wazi juu ya ugonjwa kabla ya kifo, na walikwenda mbali zai kuhusu namna ya makabidhiano ya nchi yatakuwaje.
Mkuu wa Majeshi Mstaafu nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo kupitia mahojiano yaliyofanywa na Daily News Digital amesema kuwa mijadala iliyoibuka juu ya namna ya makabidhiano ya madaraka baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, inawezekana ilitokana na baadhi ya watu kusahau Katiba inasema nini pale Rais anapofariki au kushindwa kuendelea na majukumu yake.
Itakumbukwa kwamba Jenerali Mabeyo alikuwa mkuu wa majeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzia Februari 06, 2017 na kustaafu mnamo Juni 30, 2022.
“Kwa mujibu wa Katiba, bahati nzuri imeeleza vizuri endapo Rais atafariki au endapo atashindwa kutekeleza majukumu yake kama Rais, atakayeshika madaraka ni Makamu wa Rais,”anaeleza Mabeyo. “Sasa inawezekana watu Katiba walikuwa wameisahau kidogo kukatokea maongezi tofauti.”
Mabeyo anasema anamshukuru Mungu kwa kuwa makabidhiano ya madaraka katika kipindi hiko kigumu ambacho nchi haikuwahi kukipitia yalikwenda vizuri kwa kuwa ilibidi kuhakikisha Katiba inazingatiwa.
Hata hivyo anakiri kwamba kulikuwa na ugumu uliosababisha kuchukua saa 48 kabla ya rais mwingine hajaapishwa jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Tanzania, hali iliyotokana na pande mbili kuwa kutofautiana kimaamuzi.
Anaeleza kwamba Magufuli wakati anaugua wao walishirikishwa kama Vyombo vya Ulinzi na Usalama ili wajue hali ya Rais inakwendaje wakati na wote walikuwa na ratiba ya kwenda kumuona asubuhi na jioni.
Lakini baadaye walifikia maamuzi ya kumpelekea hospitali ya Mzena kwa kuwa palikuwa na utulivu hivyo matibabu yalihamia pale na waliweza kudhibiti watu ili apate kupumzika vizuri.
Jenerali Mabeyo anasema siku moja kabla ya kifo chake hayati Magufuli alimwambia Mabeyo kwamba kupona haitawezekana hivyo alimtaka aamuru arudishwe nyumbani kama kufa akafie nyumbani.
“Siku moja kabla ya kifo chake hali ilibadilika na yeye alijitambua kwamba hali imebadilika na nadhani alijua, Mwenyezi Mungu alimuongoza kwamba hatapona, alichosema nirudisheni nyumbani nikafie nyumbani.Nikasema mheshimiwa hapana, hapa upo kwenye mikono salama, madaktari wapo waendelee kukutibu”
Mabeyo anaeleza kuwa madaktari walivyoona hali ya Rais Magufuli inabadilika waliwaita wakuu wa vyombo vya ulinzi yaani Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania, Diwani Athumani Msuya na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.
“Ilipofika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho, wakuu wa vyombo tuko pale mimi IGP na DGIS(Mkurugenzi wa Usalama),” anaeleza Mabeyo huku akisema kuwa kulikua na kigugumizi nani wa kumtaarifu wa kwanza, Rais Samia wakati huo alikua Tanga, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alikua Dodoma na Katibu Mkuu Kongozi, Bashiru Ally alikua Dodoma.
“Kwa hiyo tuliokuwa Dar es Salaam tulikuwa watatu tu, tukasema kwa kuwa Rais yuko Tanga hebu tumuambie kwanza Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi waje bila kueleza sababu, bahati nzuri wakaja mapema, sasa mimi kama mwenyekiti wa wakuu wa vyombo ilibidi nieleze Mheshimiwa Rais ameshatutoka.”
“Kwa hiyo tukaanza kushauriana tunafanyaje? Nani anatakiwa atangaze hizi habari kwenye vyombo vya habari wananchi wajue? Ndio tukaanza kutafuta Katiba sasa inasema nini?”
Mabeyo anasema kwa kuwa mtu pekee anayetakiwa kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu wa Rais ambaye alikuwa Tanga, ikabidi mawasiliano mengine yafanyike akiwa Tanga, pamoja na kutuma ujumbe kwa familia ya Magufuli.
Suala la kumuapisha Rais kuchukua saa 48
Mabeyo anakiri kwamba kikawaida ilitakiwa ndani ya saa 24 rais mpya awe ametangazwa na kuapishwa, lakini haikutokea hivyo wakati wa kifo cha Hayati Magufuli kutokana na mjadala ulioibuka kupelekea Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa baada ya siku mbili yaani Machi 19, 2021.
“Kulikuwa na mawazo mawili, aapishwe Rais baada ya kuzika au aapishwe Rais kabla ya kuzika.” amesema Mbeyo. “Lakini logic ikaja kwamba kuna marais wengine watatoka nje ya nchi kuja kumzika mwenzao watapokelewa na makamu wa rais au rais?”
Mabeyo aliendelea kusema kuwa uliibuka mjadala mwingine tena wa namna gani Rais mpya atakavyo apishwa kwa madai kuwa kusiwe na paredi kwa sababu nchi ipo kwenye msiba, kitu ambacho mkuu huyo wa majeshi mstaafu alisema gwaride lazima liwepo na bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipande kwa gwaride.
“Nikasema huyu ni Amir Jeshi Mkuu anayeapishwa, asipoapishwa kwa taratibu hizo za kitaifa Jeshi halitamtambua,” anafafanua zaidi Mabeyo.
Sambamba na hilo, ametolea ufafanuzi kwa nini siku ya uapisho wa Rais Samia alisisitiza kuwa atambulike kama ni Amiri Jeshi Mkuu na siyo ‘Amirat Jeshi Mkuu’ kama baadhi ya watu na vyombo vya habari viliyoanza kuibua mjadala.
Mjadala kuhusu cheo cha Amiri Jeshi Mkuu na jinsi yake
“Jeshini tuna afisa na askari. Hakuna mwanaume na mwanamke. Kwa hiyo hata amir Jeshi neno lile linabaki kuwa Amir Jeshi ni Commander in Chief, hiyo Amirat ni kidini,” anaendelea kueleza, “tukawauliza na BAKITA wakaeleza vizuri.”
Ni miaka mitatu sasa imetimia tangu hayati Magufuli afariki dunia akiwa madarakani ambapo ni kwa mara ya kwanza Taifa la Tanzania lilingia katika msiba huo mzito.
Magufuli alifariki katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam wakati akipatiwa matibabu kutokana na maradhi ya moyo kwa miaka 10.