Search
Close this search box.
Africa

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) Mstaafu nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, amesema licha ya kustaafu jeshini, lakini bado moyo wake ni jeshi na kwamba bado analipenda jeshi na Taifa lake. 

Mabeyo ametoa kauli hiyo katika hafla ya kumuaga iliyofanyika jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, tarehe 15 Julai 2022, ikiwa ni wiki kadhaa tangu astaafu jeshi tarehe 30 Juni 2022.

“Niko jeshini miaka mingi, hata ukichanja damu yangu ni jeshi. Nimetoka jeshini, moyo wangu bado ni jeshi na utaendelea kuwa jeshi. Bado nalipenda jeshi na nalipenda Taifa langu, nitaendelea kulitumikia mpaka mwisho,” amesema Jenerali Mabeyo.

Ameongeza kuwa “nimejisikia nafuu kidogo, unajua kila siku nilikuwa nawaza naenda ofisini kuna majukumu gani, sasa hivi hiyo imetoka. Sasa nafikiri niishi namna gani na wananchi wenzangu.”

Jenerali Mabeyo amewataka Watanzania waipende Tanzania, ili wawe na moyo wa kuitumikia kwa ajili ya kuiletea maendeleo.

“Mimi nimestaafu lakini moyo wangu ni Tanzania na mimi nawashauri Watanzania kuipenda Tanzania. Ukiipenda Tanzania utaitumikia na ndiyo itapata maendeleo, kama huipendi Tanzania hata moyo wako wa kiutendaji utakuwa wa chini sana na dhaifu. Niwase Watanzania waipende Tanzania,” amesema Jenerali Mabeyo.

Comments are closed