Jezi ambayo nguli wa soka wa Argentina, Diego Maradona alivaa alipofunga mabao mawili dhidi ya Uingereza katika Kombe la Dunia la 1986, likiwemo bao maarufu la ‘Hand of God’ ilipigwa mnada kwa dola milioni 9.3, rekodi ya bidhaa zozote za kumbukumbu za michezo, kampuni yam nada ya Sotheby’s ilisema Jumatano.
Wazabuni saba walishindania vazi hilo katika mnada ulioanza Aprili 20 na kumalizika Jumatano asubuhi, Sotheby’s ilisema.
“Jezi hiyo ya kihistoria ni ukumbusho unaoonekana wa wakati muhimu sio tu katika historia ya michezo, lakini katika historia ya karne ya 20,” mkuu wa kampuni ya Streetwear Brahm Wachter alisema katika taarifa baada ya mauzo.
“Hii bila shaka ndiyo jezi ya soka inayotamaniwa zaidi kuwahi kupigwa mnada, na hivyo sasa inashikilia rekodi ya mnada wa kitu chochote cha aina yake,” alisema.
Jezi hiyo ilikuwa inamilikiwa na kiungo pinzani Steve Hodge, ambaye alibadilishana jezi yake na Maradona baada ya Uingereza kufungwa 2-1 huko Mexico City.
Binti ya Maradona alitilia shaka mauzo hayo mapema mwezi huu alipodai kuwa jezi iliyopigwa mnada ni ile ambayo babake alivaa kipindi cha kwanza ambapo babake hakufunga bao, na sio cha pili alipofunga mabao yake mawili.
Sotheby’s alisisitiza kuwa walikuwa na jezi sahihi.
Rekodi ya awali ya jezi iliyouzwa kwa kima cha pesa nyingi katika mchezo wowote ilikuwa dola milioni 5.6, iliyowekwa mwaka wa 2019 kwa jezi aliyovaa Babe Ruth alipokuwa New York Yankees.