Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete na makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi ccm, Abdurahman Kinana wamemuandikia barua mhariri wa gazeti la Mwanahalisi, Said Kubenea wakimtaka kuomba radhi dhidi ya taarifa iliyochapwa na gazeti hilo Julay 20, 2023.
Viongozi hao pia wamemtaka Kubenea kutoa kiapo cha kisheria, kwamba yeye na gazeti analolihariri wanaahidi kuacha kuwakashifu, kutoa namna yoyote ya lugha isiyofaa, maneno ya uongo, kero au uchafuzi dhidi yao, na endapo wakishindwa hatua za kisheria zitachukuliwa.
Kwa mujibu wa barua ya Wakili Eric S. Ng’maryo iliyokwenda kwa Kubenea na kampuni ya Hali Halisi Publishers imesema Gazeti la MwanaHalisi toleo la Julai 20 hadi 26, mwaka huu limechapisha taarifa kuwa Kikwete na Kinana wamekuwa wakiwalipa watu fedha ili waendelee kupinga uwekezaji wa bandari jambo ambalo linawadhalilisha viongozi hao.
Barua ya viongozi hao hiyo iliyoandikwa na kampuni ya wakili Eric s. Ng’maryo inamtaka mhariri wa Gazeti hilo Said Kubenea kufuta kashfa dhidi ya viongozi hao na kuomba radhi ndani ya siku 14, la sivyo watachukua hatua za kisheria.
Barua hiyo ya madai imeeleza kiini cha kashfa hiyo ni tuhuma za uongo kwamba viongozi hawa wanachochea wale wanaopinga maendelezo ya bandari kwa kuwalipa fedha watu ambao hawajatajwa ili watu hao wapinge au waendelee kupinga maendelelezo ya bandari.