JWTZ yatoa tahadhari dhidi ya matapeli

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wananchi kupuuza taarifa za baadhi ya watu waliowaita matapeli ambao wamekuwa wakiwalaghai wananchi fedha zao kwa kigezo cha kuwapa nafasi za kazi katika jeshi hilo.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 30, 2021 na msemaji wa Jeshi hilo, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema vitendo hivyo vimeleta usumbufu ambapo matapeli hao husingizia viongozi, makamanda wa Jeshi kwamba wametumwa wakusanye hela ili kuandikisha vijana hao.

“Niwaombe Watanzania wawapuuze na kamwe wasidanganyike kutoa fedha ili kupata nafasi Jeshini, hakuna nafasi ya kuingizwa jeshini kwa kutumia mgongo wa fedha na nitoe rai kwa wanaofanya vitendo hivyo vya ulaghai waaache” amesema Luteni Ikonda.

Luteni Ikonda amesema matapeli hao wanakodi gesti na kukusanya vijana kisha kuwadanganya kuwa watawapa kazi jeshini na baada ya hapo wanawatelekeza, hali inayofanya wazazi kwenda jeshini kuuliza kwa Mkuu wa Majeshi

 “ wazazi wanakuja Jeshini kuuulizia kwa mkuu wa majeshi na wakiambiwa lete hiyo namba ukipiga inajibiwa haipatikani” ameongeza Luteni Ikonda.

Luteni Ikonda amesema Jeshi lina taratibu na miongozo yake kwa vijana wanaotaka kujiunga na sio kigezo cha fedha kama ambayo matapeli hao wamekuwa wakifanya.