Mwandishi wa Habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera, amesema anakusudia kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini humo kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam, ambayo ilitupilia mbali shauri lake namba 12799/2024, aliyoifungua dhidi ya kampuni ya huduma za mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.
Kabendera ametoa kauli hiyo jana Oktoba Mosi 2024, kupitia video yake fupi kwa vyombo vya habari ambapo ameeleza kuwa tayari ameshawasiliana na mawakili wake, waliopo nchini Uingereza na Afrika Kusini ambao ndio wanaomsimamia katika kesi hiyo.
“Tutakata rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania dhidi ya pingamizi lililowekwa dhidi yangu, kwakuwa mimi na wanasheria wangu tunaamini kuwa kesi yetu ina mashiko na inastahili kusikilizwa”- amesema Kabendera
Itakumbukwa kuwa mnamo Septemba 10,2024 Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ilifuta kesi hiyo baada ya mahakama kusikiliza pingamizi la awali lililowekwa na Vodacom.
Katika kesi hiyo Kabendera aliyewakilishwa na Wakili Peter Madeleka alikuwa akiituhumu Vodacom kufanikisha kukamatwa kwake akieleza kama ‘kutekwa’ na hatimaye kufunguliwa kesi hiyo ya uhujumu Uchumi mwaka 2019.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ilisababisha madhara makubwa kwake, yakiwemo ya kiuchumi, kijamii, kisaikolojia, kutokufurahia Maisha na hadhi yake kwenye jamii, ambapo aliwasilisha madai ya fidia ya Dola za Marekani milioni 10 (TZS bilioni 28) kama fidia kwa hasara alizodai kupata kutokana na tukio hilo pamoja na riba kutoka tarehe ya hukumu hadi malipo yatakapokamilika.
Hata hivyo, Vodacom imefanikiwa kupinga kesi hiyo ambapo Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Livin Lyakinana kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo kutoa uamuzi wa kuifuta.
Kabendera amesema hoja ya kufutwa kwa kesi yake kwa maelezo ilifunguliwa nje ya muda, ni kwa sababu alitoka gerezani akiwa mgonjwa na kipaumbele chake na familia yake kilikuwa ni matibabu yake kutokana na afya yake kuonekana kudhoofika baada ya kutoka gerezani.
“Nilipotoka jela nilikuwa nadaiwa kiasi kikubwa cha fedha; pili hali yangu ya afya ilikuwa ya mashaka kiasi iliwapa wasiwasi ndugu zangu kwa hiyo kipaumbele cha kwanza kilikuwa afya yangu, lakini kuhusika kwa mtandao wa Vodacom kwenye utekwaji wangu kupo wazi,” amesema.
Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake, Mbweni jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na kushikiliwa kwa siku kadhaa, kisha akafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ilimalizika kwa utaratibu wa majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), unaojulikana kisheria kama plea bargaining.
Aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kulipa fidia ya hasara aliyodaiwa kusababisha kwa kukwepa kodi zaidi ya Sh. 173 milioni na faini aliyoamuriwa na Mahakama baada ya kumtia hatiani kwa kukiri makosa yake kulingana na majadiliano na makubaliano hayo na DPP.
Katikati ya mwaka huu, ikiwa ni miaka mitano baada ya kukamatwa na miaka minne baada ya kesi yake hiyo ya uhujumu uchumi kumalizika, ndipo Kabendera akafungau kesi hiyo ya madai ya fidia dhidi ya Vodacom.
Katika kesi hiyo, Kabendera alieleza kuwa simu yake, ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kuwasiliana, kabla ya tukio la kukamatwa kwake.
Pia, Kabendera alieleza juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo, kwa kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo, lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake ambayo alikuwa ameizima tangu jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaimi kuwa haikuwa na mtandao.
Hivyo, aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja, kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.
Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza kuwa namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796), ilikuwa na changamoto za kiufundi ambayo ilimhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.
Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa akidai ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.
Hata hivyo (Kabendera alisita kwenda kituo cha huduma kwa wateja), kwa kuwa kulikuwa kina matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016.
Kabendera alidai, Jumatatu ya tarehe 29 Julai 2019 saa 4:00 asubuhi, alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akimlalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa pesa kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.
Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza kuwa asubiri kidogo ili amuulize meneja wake, na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mliman City asubuhi hiyo.
Hata hivyo saa 9:00 alasiri siku hiyo hiyo ya Julai 29, ghafla tu simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipoigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom, ambaye alimtaka (Kabendera), amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumuelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo.
Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom, ambayo aliipokea akabaini kuwa ilikuwa ni sauti ya mwanamume, ambaye alimtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikihanikiza na kukwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa
Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabendera, akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliweza kuona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake
Kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegesha mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake, halafu wakashuka watu wanne ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa polisi, lakini walikataa kutoa utambulisho. Walimpiga pingu kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.
Kabendera analalamika polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais (wa wakati huo), John Magufuli