Kada wa Chadema aliyetoweka na kukutwa polisi apandishwa kizimbani kimya kimya na kusomewa mashtaka matatu

Kada wa Chadema, Kombo Mbwana aliyetoweka kwa siku 29 na kubainika kushikiliwa na Polisi, jana Julai 16, 2024 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga na kusomewa mashtaka matatu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya kesi namba 19759/2024, Kombo ameshtakiwa kwa makosa matatu ambayo ni pamoja na kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume cha kifungu 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika kosa hilo, inadaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa akimiliki laini ya Tigo ikiwa na namba (ICCID), 8925502042093621824 iliyosajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umilikiwa wa laini hiyo.

Shitaka la pili, ni kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na mtu mwingine kinyume cha Kanuni ya 4(1)©, 12(3) na 21(1) ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Kanuni za usajili wa laini za simu) za mwaka 2020 zikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 52 cha Sheria ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Sura ya 306 RE 2022).

Katika shtaka hilo inadaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa alikutwa akimiliki laini ya laini ya Tigo yenye ICCID 8925502042093621824 ya namba 0719 672 633 ambayo awali ilikuwa ikimiliwa na mtu aliyesajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa, bila kusajili namba hiyo kwa mamlaka.

Imedaiwa Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga, Kombo alikutwa alikutwa akimiliki laini ya laini ya Tigo yenye ICCID 8925502042093621824 ya namba 0719 672 633 iliyokuwa ikimilikiwa na mtu aliyesajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa bila kujulisha mamlaka.

Dhamana ya kesi hiyo ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanataosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja na barua ya mtendaji wa mtaa na vitambulisho vya Taifa (Nida). Mshtakiwa ameshindwa kutumiza masharti ya dhanama, amepelekwa mahabusu.

Shitaka la tatu kwa mujibu wa hati hiyo ni kushindwa kuripoti mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu kinyume cha 4(1) © na 21(1) ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Kanuni za usajili wa laini za simu) za mwaka 2020 zikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 152 cha Sheria ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Sura ya 306 RE 2022).

Kombo aliyetoweka tangu Juni 15, 2024 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake katika Kijiji cha Komsala Handeni mkoani Tanga, alibainika kushikiliwa na Polisi, baada ya Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Zacharia Bernard kutoa taarifa Julai 14, 2024 akieleza kumshikilia kwa tuhuma za kutumia vifaa vya kielektroniki pamoja na laini za simu zisizosajiliwa katika kutekeleza uhalifu, kinyume cha sheria za nchi.

Hadi taarifa ya Jeshi la Polisi kukiri kumshikilia Kombo tayari zilikuwa tayari zimepita siku 29, tangu atoweke na hii ni baada ya kelele mitandaoni zikihamasisha kujua wapi alipo Kombo.

Hata hivyo hata baada ya kupatikana kwake na polisi kukiri kumshikilia ndugu wa Kombo pamojana mawakili walizuiwa kumuona tangu Julai 15 hadi jana aliporuhusiwa mama mzazi wa Kombo kwenda kumuona na baadae kupelekwa Mahakamani kinyemela.

Matukio ya utekaji na watu kutoweka na baadae kuonekana katika mazingira tata yameibua maswali mengi kwa wananchi huku yakihusishwa na Jeshi la Polisi kutokana na kauli zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Hata hivyo Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillius Wambura limekana tuhuma hizo na kusema kwamba jeshi hilo halihusiki na utekaji, bali limekuwa likiwaokoa wanaotekwa.

Tukio la kutekwa kwa Kombo lililotokea Juni 15, 2024 kijijini kwao Kwamsala wilayani Handeni, Tanga ambapo watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake wakidai eneo analojenga nyumba yake ni la kwao.