Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amewasili Dar es Salaam nchini Tanzania usiku wa Jumatano kwa ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini humo
Alikaribishwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Phillip Mpango katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Ndege ya Air Force Two, toleo maalum la C-32 ya Boeing 757-200 iliwasili Tanzania kutoka Ghana ambako Bi Harris alitumia siku tatu za kwanza za ziara yake barani Afrika. Pia anatarajiwa kuzuru Zambia kabla ya kusafiri kwa ndege kurudi Marekani.
Ziara hii ya kiserikali inatokana na mwaliko wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, wakati walipokutana jijini Washington mwaka 2022, ikitajwa pamoja na mambo mengine kuwa ni kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, sambamba na kuzungumzia maendeleo ya uchumi, mabadiliko ya tabia nchi.
Wawili hao wakiwa na historia kwenye mataifa yao kuwa viongozi wanawake wa kwanza, watakuwa na mazungumzo na pia jioni atashiriki futari aliyoandaliwa na mwenyeji wake.
Marekani ni miongoni mwa mataifa yanayofanya vizuri kwenye uwekezaji nchini Tanzania ambapo hadi sasa miradi 266 ya Marekani imesajiliwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na thamani ya Dola 4.778 bilioni.
Itakumbukwa kuwa Ushirikiano wa Marekani na Tanzania ulianza mwaka 1961,na ilipofika mwaka 1968 nchi hizo ziliwekeana saini kwenye mikataba kadhaa ya ushirikiano na hadi sasa uhusiano huo unazidi kuimarika zaidi.