Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Patrobas Katambi amesema vijana wote wamepata mikopo kupitia halmashauri na ambaye hajapata huenda ni Mkenya.
Katambi amesema hayo leo Mei 18, 2022 bungeni mjini Dodoma, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, aliyehoji vijana kutopata ajira kwa zaidi ya miaka sita sasa pamoja na kwamba kuna mfumo wa utoaji wa mikopo katika halmashauri , hivyo mfumo huo unawatupa nje.
“Ukiangalia hakuna kijana yeyote ambaye hapati mkopo, kumekuwa na scheme za utoaji mkopo katika elimu, sekondari tumekuwa tukitoa elimu bila malipo, chuo kikuu anakutana na Bodi ya Mikopo, akitoka chuo akienda kwenye halmashauri zetu tunatoa mikopo.
“Pia tumekuwa na scheme za makubaliano na mabenki mbalimbali kushusha riba na kutoa mikopo, kama mtapitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, kule kuna mpango wa ‘Building the better tomorrow’ utakaogusa zaidi ya vijana milioni 1, ili kutengenezewa scheme za kilimo,” amesema.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na Mwakagenda, ambaye alisema: “Mhe. Naibu Waziri (Katambi), unavyoeleza ni kama vile uko nje ya Tanzania, tuna vijana wengi sana wamekosa ajira zaidi ya miaka sita sasa, umesema kwenye halmashauri kuna nafasi za wao kupata pesa, vijana wengi mfumo unawaacha nje.”
Katika swali la nyongeza Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alihoji ni kwa nini serikali isiandae mfumo mzuri wa kuwakopesha vijana wasiokuwa na ajira wale wanaotaka kuingia kwenye ujasiriamali wakakopeshwa hata walau mtaji wa Sh Milioni 20 wa kuanzia na wakajidhamini kwa vyeti vyao vya chuo
Akijibu swali hilo, Katambi alisema zaidi ya Sh bilioni 150, zimekwishatolewa kwa vijana kama mikopo na kama kuna kijana yeyote ambaye hajapata mkopo itakuwa pengine ni Mkenya.
“Sisi kama serikali tunazo takwimu za vijana hawa, na wale wote wanaofanya application za ajira, vyuo vikuu vyote tumekuwa tukipata taarifa, tunao vijana zaidi ya 200,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kutoka vyuo mbalimbali.
“Pia tuna mifumo na programu tunazoziandaa ikiwa ni pamoja na ‘internship’, kuangaliziwa ajira ndani na nje ya nchi,”amesema Katambia na kuongeza:
“Tumekuwa tukiendelea kutoa mikopo na zaidi ya Sh bilioni 150 zimekwishatolewa kwa vijana mbalimbali, kama kuna vijana ambao wapo labda pengine sio Watanzania ni Wakenya utanisaidia niweze kuwaingiza hapa tuone namna gani tunawasaidia.”