Search
Close this search box.
Africa

Hoja ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi imepamba mkutano wa baraza kuu la CHADEMA nchini Tanzania, baada ya kuwekewa mkazo na msisitizo huku serikali ikitakiwa isogope michakato hiyo.

Katika mkutano huo ambao uliwakutanisha pia wanasiasa wa siasa za upinzani kutoka ndani na nje ya Tanzania, wanasiasa hao kwa nyakati tofauti wamesema kuwa hoja hizo zinapaswa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Akizungumzia kuhusu Tume Huru ya uchaguzi mwenyekiti wa chama cha ACT – Wazalendo Juma Duni Haji amesema kama chama wao dhamira yao kuu ni Tume Huru ya uchaguzi lakini kuhusu Katiba Mpya ni ajenda pia ya kuipigania na wako tayari kushirikiana na vyama vingine katika kudai Katiba Mpya.

“Kazi yetu sisi wana siasa ni kuaandaa umma ili watawala wajue mbivu kama sio mbichi, sisi vyama wa upinzani tunapaswa kuunganisha nguvu na kuwa wamoja.Tunahitaji tukitoka hapa tunaenda kwa wananchi, salamu yetu iwe Katiba mpya na hao ndio wanaotakiwa kuelimishwa ili watuunge mkono,” amesema Duni

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chama cha Wananchi CUF Salvatory Magafu, ambaye pia alipata mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo amesema msingi wa Katiba mpya ni kwenda kuiondoa sheria kandamizi zilizopo sasa ambazo zinaweka mazingira magumu ya kisiasa.

Itakumbukwa kua Novemba 2, 2020 chama hicho kilikaa na kuadhimia kutoshiriki uchaguzi wowote hadi itakapopatikana katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi.

Aidha Mwenyekiti wa chama cha CHAUMA, Hashimu Rungwe amesema suala la Katiba mpya haliepukiki na kwamba hiyo ndio mzizi wa fitina.

“Katiba ndio mzizi wa fitna, CHAUMA kilio chake ni katiba mpya, hakuna kitu kingine tunachotaka na watu wote tukae hapo” amesema Rungwe.

Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa CHADEMA amesema suala la Katiba mpya ni suala ambalo halina mjdala na kwamba ajenda ya Tume Huru isikwamishe mchakato wa madai ya katiba Tanzania

“Ajenda ya Tume Huru haipaswi kusimamisha mchakato wa katiba mpya, haya mambo yanapaswa kutegemeana na kwenda pamoja, mchakato wa Katiba hauna mjadala”-amesema Mbowe

Ameongeza kuwa kama kuna mabishano ya ajenda hizo yafanyika kwa kujenga hoja na si kuhusu maudhui gani yanapaswa kuwepo.

“Tunataka katiba na kama tunabishana kuhusu katiba basi tubishane kwa hoja kuhusu maudhui yanayopaswa kuwemo kwenye katiba. Sisi CHADEMA pekee hatuwezi kutengeneza katiba, hivyo hivyo kwa CCM na vyama vingine, ni lazima tuungane wote ili kupata katiba”

Kwa sasa nchini Tanzania kunaendelea vuguvugu la madai ya Katiba mpya na Tume Huru ya uchaguzi, kutokana na madai kwamba tume na katiba iliyopo sasa haina uhuru katika vipengele vingi vya sheria hali inayofanya kukandamiza vyama vya siasa.

Hata hivyo serikali iliyopo mamlakani imesema kwa sasa inajenga nchi katika kuwaletea maendelea wananchi wake na suala la ajenda ya katiba na tume huru sio kipaumbele 

Comments are closed