Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu nchini Tanzania (CWT), Deus Seif na Mwekahazina wa chama hicho, Abubakari Allawi, wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha shilingi milioni 13.9 mali ya CWT.
Hukumu hiyo imesomwa jana usiku Juni 28, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi yao ya uhujumu uchumu namba 39/2021 ilipoitwa.
Akitoa Hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate amesema mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao na kila mmoja atatumikia kifungo cha miezi sita jela.
” Mbali na adhabu hii, mshtakiwa kwa kwanza(Seif) utakapomaliza kutumikia kifungo chako utatakiwa kuilipa fidia CWT ya shilingi milioni 7,590,000, kwa upande wa mshtakiwa wa pili (Allawi) wewe utakapomaliza kutumikia kifungo hicho utatakiwa kuilipa fidia CWT kiasi cha shilingi milioni 6.2, haki ya kukata rufaa ipo wazi” amesema Hakimu Kabate.
Awali, jopo la mawakili watatu kutoka Takukuru wakiongozwa na Iman Nitume, waliomba Mahakama hiyo itoa adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao kwa mujibu wa sheria walivyoshtakiwa nayo.
” Kulingana na makosa waliyotenda na uhalisia wa nafasi za uongozi walizokuwa nazo CWT, ambapo waliaminiwa na walimu ambao walikuwa wanatoa michango yao kwa ajili ya chama hicho lakini wao walitumia hela za chama kwa maslahi yao binafsi” amedai wakili Nitume.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa utetezi Nesto Mkoba aliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu wateja wake kwa sababu ni wagonjwa, wanategemewa na familia zao na pia wanawahudumia wazazi wao wenye umri zaidi ya miaka 80.
Katika kesi ya msingi, Seif na Allawi, wanadaiwa kati ya Oktoba 3, 2018 na Novemba 6, 2018, katika ofisi za CWT zilizopo Kinondoni, wakiwa waajiriwa wa chama hicho, walitumia Mamlaka yao vibaya kwa kujipatia shilingi milioni 13, 930,693.
Shtaka la pili, siku na maeneo hayo, Seif na Allawi, kwa kutumia madaraka yao vibaya na kwa manufaa yao wenyewe wanadaiwa kuchepusha fedha kiasi cha shilingi milioni 13.9 ambayo ni mali ya CWT.
Viongozi hao wanadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipia tiketi za ndege pamoja na kulipia gharama za malazi kwa ajili ya safari ya kwenda Cape Verde kuangalia mpira wa miguu.
Inadaiwa kuwa mwaka 2018, huko Cape Verde kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), waliokuwa wanacheza na Timu ya Taifa ya Cape Verde.
Washtakiwa kwa kufanya hivyo, wanadaiwa kwenda kinyume na vifungu vya 29 pamoja na 31 vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.