Kaya 25 kuwasili Msomera leo

Jumla ya kaya 25 za wananchi wa Ngorongoro mkoani Arusha, wanatarajiwa kupokelewa leo wilayani Handeni mkoani Tanga katika kijiji cha Msomera ikiwa ni muendelezo wa wale ambao wamekubali kuhama kwa hiari.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba amesema hayo jana Alhamisi Agosti 18, 2022 kwenye ziara yake ya kukagua maandalizi ya kupokea kaya 25 katika kijiji cha Msomera na kusema kuwa mpaka sasa maandalizi ya kuwapokea wananchi hao yapo tayari ambapo zaidi ya nyumba 25 zimekamilika.

Amesema nyumba hizo zinatakiwa kukabidhiwa Septemba 30 lakini Suma JKT kwa umahili wao katika kazi, wameshaanza kumalimiza baadhi ya nyumba na tayari wananchi wanaweza kuhamia.

“Nimefarikijika zaidi mkuu wa kikosi na wanajeshi kwa ujumla kunipa taarifa kuwa mpaka Agosti 30 watakuwa wamemaliza mradi huu wa nyumba 402, watakabidhi nyumba ya askari,kituo cha polisi na majengo mengine kwa muda muafaka”, amesema Mgumba.

Lakini pia kuagiza haraka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga kupeleka polisi katika eneo hilo mapema mwezi ujao, baada ya kituo cha polisi cha Msomera kukamilika lengo ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakamilika.

Luteni kanali Edward Mwanga msimamizi wa ujenzi wa nyumba hizo mpya amesema nyumba 25 zipo tayari ila wameongeza nyingine nne na kufanya idadi kufikia 29, hivyo kaya 29 zinaweza kupokelewa muda wowote.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Sofia Jongo amewahakikishia usalama wananchi hao na kusema kuwa watafanyiakazi agizo la mkuu wa mkoa la kupeleka polisi kwenye kituo kipya,ila kuomba msaada wa gari kwaajili ya kituo hicho.

Mwenyekiti wa wananchi hao, Samwel Daniel amesema mpaka sasa wameridhishwa na mazingira ya Msomera na kushauri wengine kujiandikisha ili kuweza kuhamia hapo na hakuna changamoto kama wengine wanavyosema.