Kutoka kazi za benki hadi kazi katika mashirika ya kimataifa, mitandao ya kijamii barani Afrika imejaa ofa za kazi nzuri.
Lakini wachunguzi wa AFP Fact Check wamegundua kuwa mengi ya matangazo haya ni ya uwongo — ni ulaghai ulioundwa ili kuibia watu pesa au kuiba data ya kibinafsi.
Akiwa amemaliza chuo kikuu nchini Kenya — nchi iliyo na vijana zaidi ya milioni 1.6 wasio na ajira — Job Mwangi aliamini kuwa alikuwa ameorodheshwa kuwa msaidizi wa nyanjani katika Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), nafasi iliyotangazwa kwenye LinkedIn.
Baada ya kufaulu usaili mara mbili mtandaoni, aliombwa kulipa shilingi 2,000 za Kenya kama ‘ada za uwezeshaji’ ili afanyiwe usaili.
“Kila kitu kuhusu tangazo hilo la kazi ilionekana kuwa halali,”
“Nilitakiwa kulipa shilingi 1,000 za Kenya kwa ajili ya vipimo vya matibabu na radiolojia… lakini vipimo havikufanyika tangu nilipoambiwa kwamba vingefanyika katika ofisi za Umoja wa Mataifa siku ya mahojiano.”
Basi la abiria ambalo lilipaswa kumhamisha Mwangi na watu wengine zaidi ya 30 wanaotafuta kazi katika ofisi ya Umoja wa Mataifa halikuwahi kufika.
“Tulisubiri basi la Umoja wa Mataifa kwa takribani saa moja lakini halikufika, hivyo tukaamua kupanda basi wenyewe.
“Tulipofika getini, tulitaja kuwa tumealikwa kwa mahojiano na UNEP na maafisa wa usalama. Msimamizi wa lango alitucheka, na kutuambia kwamba tumetapeliwa.” Mwangi aliwasilisha ripoti kwa polisi lakini anasema hajasikia lolote tangu wakati huo.
Udanganyifu huu ni jambo la kawaida barani Afrika — hakika, mashirika ya Umoja wa Mataifa huwaonya wanaotafuta kazi mara kwa mara kuhusu matangazo ghushi.
“Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa haitozi ada katika hatua yoyote ya mchakato wake wa kuajiri (maombi, mahojiano, usindikaji, mafunzo) au ada nyinginezo, au kuomba taarifa kuhusu akaunti za benki za wanaomba kazi” UNEP inasema kwenye tovuti yake.
Upekuzi kwenye Facebook hufichua kurasa nyingi zilizo na nafasi ghushi zilizobuniwa kwa ustadi ili kuvutia watu wanaotafuta kazi.
Matangazo mengi ya nafasi za ajira zina dalili zinazofanana: zina makataa mafupi, huahidi mishahara mikubwa na mara nyingi hujumuisha kiungo kwenye jukwaa la nje la mtandao linaloomba maelezo ya kibinafsi.
Walaghai pia hutumia nembo za mashirika na kampuni zinazotambulika ili kuonyesha kuwa kampuni zao ni halali.
Code for Africa, uandishi wa habari za data na mpango wa teknolojia ya kiraia, uligundua kuwa mnamo 2020 — wakati upotezaji wa kazi uliongezeka wakati wa janga la Covid-19 — akaunti 30 za Facebook, vikundi na kurasa zenye wafuasi zaidi ya 184,000 zililenga wanaotafuta kazi nchini Kenya kwa kyutumia matangazo feki.
Wachambuzi wanasema wanaohusika na ulaghai huu wanategemea waliovunjika moyo katika kupata kazi ambao mara nyingi hushindwa kuangalia kama matangazo hayo ni ya kweli.
Wengi ya wale wanaotafuta kazi hutuma pesa bila kusita, wakitumai hii itawasaidia katika kinyang’anyiro cha kupata nafasi hiyo.
“Ulaghai mwingi wa kazi mtandaoni unalenga kuwalaghai watu kutuma pesa na pesa hizi zikishatumwa tapeli hutoweka,” mtaalam wa usalama wa mtandao wa Kenya Anthony Muiyuro aliambia AFP Fact Check.
LinkedIn ilisema ilikuwa inawekeza katika njia za kukabiliana na tatizo hilo.
“Timu zetu hutumia ulinzi wa kiotomatiki kugundua na kushughulikia akaunti ghushi au ulaghai unaoshukiwa. Pia tunawahimiza wanachama kuripoti jambo lolote ambalo linaonekana si sawa ili tufanye uchunguzi,” kampuni hiyo iliiambia AFP Fact Check.
Nchi nyingine zinazolengwa barani Afrika ni pamoja na Nigeria, taifa lenye watu wengi zaidi barani humo, ambapo zaidi ya milioni 23 hawana ajira.