Kesi ya jinai namba 25480 ya mwaka 2025, iliyofunguliwa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake wawili (Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu), dhidi ya viongozi waandamizi wa chama hicho wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake wa Tanzania Bara, John Heche, imetajwa leo mahakamani hapo chini ya Jaji Awamu Mbagwa.
Katika kesi hiyo, vigogo hao wa CHADEMA wanatuhumiwa kukiuka amri ya Mahakama Kuu iliyotolewa Juni 10, 2025, kufuatia uwepo wa kesi ya madai inayohusu usawa kwenye mgawanyo wa mali ndani ya CHADEMA, inayosikilizwa chini ya Jaji Hamidu Mwanga. Wadaiwa kuwa wamepigwa marufuku kujihusisha na shughuli zozote za kisiasa na matumizi ya rasilimali za chama hadi pale kesi hiyo itakapopatiwa uamuzi.
Leo mahakamani, upande wa mashtaka umewasilisha flash ambazo zinaonyesha picha jongefu (video) zinazoonesha kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti kupitia majukwaa mbalimbali, ambazo zinadaiwa kuwa ni ukiukaji wa amri ya Mahakama ya Juni 10, 2025.
Hata hivyo, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa rasmi Oktoba 22, 2025, saa 05:00 asubuhi, kutokana na kile kilichoelezwa na Mahakama kuwa imefunguliwa kwa hati ya dharura. Wakati huo, maombi ya haraka yamewasilishwa ili kuhakikisha baadhi ya watuhumiwa ambao hawajafikishwa taarifa ya kesi wanapatiwa taarifa hiyo.
Upande wa utetezi umetakiwa kuwasilisha kiapo kinzani hadi kufikia Oktoba 21, 2025. Hadi kufikia leo, ni washtakiwa watatu (3) pekee ambao wamepatiwa taarifa ya uwepo wa kesi hiyo, ambao ni John Mnyika, Bodi ya Wadhamini, na Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambapo wahusika hao wamefika mahakamani sambamba na mawakili wao Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.
Hata hivyo, washtakiwa ambao hadi leo walikuwa hawajapata taarifa hiyo na hivyo Mahakama kuagiza wapatiwe haraka ni pamoja na John Heche, Rose Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya, na Gervas Lyenda.
Upande wa mashtaka umewakilishwa na mawakili wawili (2), Shaban Marijani na Alvan Fidelis, ambao wamehudhuria kesi hii kuanzia mwanzo.