Baada ya siku kadhaa za kusikilizwa kwa ushahidi uliosheheni utaalam na hoja za kisheria, Mahakama Kuu leo ilishuhudia kukamilika kwa ushahidi wa shahidi wa tatu katika kesi ya Tundu Lissu, huku upande wa Jamhuri ukitarajiwa kuendelea kesho kwa kumuita shahidi wa nne.

Leo upande wa Jamhuri ulihitimisha kumuuliza shahidi maswali juu ya maelezo yake ya ushahidi, hatua ambayo ilitoa fursa kwa mshtakiwa Tundu Lissu kuuliza maswali ya kina kwa shahidi huyo.
Upande wa mashtaka ulianza kwa kutangaza kuwa wamehitimisha kumuhoji shahidi wao wa tatu, na jopo la majaji liliruhusu upande wa utetezi kuanza hatua ya cross-examination.
Lissu alitumia muda mwingi kumuuliza shahidi maswali kulingana na maelezo yake ya ushahidi na uhalali wa maelezo hayo
.Lissu: Sasa Shahidi, naomba uieleze Mahakama kama uliandika maelezo polisi ya ushahidi wako.
Shahidi: Sahihi, niliandika maelezo
Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba uliandika maelezo hayo tarehe 8 Oktoba 2025 katika makao makuu ya Tume ya Uchunguzi wa Kisayansi?
Shahidi: Kweli
Baada ya kuthibitisha utambulisho wa maelezo hayo, Lissu aliomba Mahakama yapokee kama kielelezo, na shahidi alikubali. Hatimaye, Mahakama ikapokea maelezo hayo rasmi kama Kielelezo D2.
Baada ya hatua hiyo, Lissu alianza kuuliza maswali ya mfululizo kuhusu mambo ambayo shahidi aliyasema mahakamani lakini hayapo kwenye maelezo yake ya polisi.
Lissu: Kwenye ushahidi wako ulisema wewe ni mtaalamu wa picha ulieteuliwa na kuthibitishwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali GN 745 la mwaka 2020. Hayo yapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Shahidi: Hayapo.
Lissu: Ulisema kati ya mwaka 2013 na 2014 ulihudhuria mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi, kweli si kweli?
Shahidi: Kweli.
Lissu: Na hayo mafunzo yapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Shahidi: Hayapo.
Lissu: Kwenye ushahidi wako hapa Mahakamani umesema ulisomea masomo kama Criminal Law, Self Defense, na Medani za Kivita, hayo yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi:Hayapo.
Kwa kila swali lililoulizwa, shahidi alionekana kushikilia msimamo wake kwamba mambo mengi aliyoyasema mahakamani hayakuandikwa katika maelezo yake ya awali. Lissu aliendelea kuchimba zaidi.
Lissu: Ulisema baada ya kumaliza hayo mafunzo mwaka 2014 ulizawadiwa cheti cha Competence na kupandishwa cheo. Hayo yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi:Hayapo alisema shahidi.
Lissu:Ulisema baada ya kupandishwa cheo kuwa Polisi Konstebo ulipangiwa kitengo cha uchunguzi wa kisayansi, hayo yapo?
Shahidi Hayapo.
Lissu:Kwenye ushahidi wako ulisema kati ya mwaka 2021 na 2022 ulihudhuria mafunzo ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, hayo yapo kwenye maelezo yako ya polisi?
Shahidi: Sikuyasema.
Lissu:Ulisema ulihudhuria mafunzo hayo kwa miezi minne na ulipomaliza ulipata cheti cha mahudhurio na kupandishwa cheo cha Assistant Inspector, hayo yapo?
Shahidi: Hayo maelezo hayapo.Baada ya mahojiano marefu kuhusu video, Lissu alibadilisha mwelekeo na kuanza kuuliza kuhusu namna maelezo ya polisi huandikwa.
Lissu: Hivi nyie polisi nani anawafundisha kuandika maelezo
Shahidi: Tunafundishwa na polisi wenzetu.
Lissu: Uliandika maelezo yako chini ya kifungu cha sheria gani?
Shahidi: Chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Lissu:Kifungu hicho kinakuruhusu kuandika maelezo yako mwenyewe
Shahidi: Mimi si mtaalamu wa sheria.
Katika hatua hiyo, Lissu alisema kwa mujibu wa hesabu zake, shahidi aliulizwa maswali 165 wakati wa ushahidi wa upande wa mashtaka, na kati ya hayo, majibu 112 hayamo kwenye maelezo yake ya polisi.
Shahidi: Sina uhakika nalo hilo.
Baada ya upande wa utetezi kumaliza, upande wa Jamhuri ulipata nafasi ya kumuuliza shahidi maswali ya kusawazisha. Wakili wa Serikali alimuuliza: “Uliulizwa kwanini hukueleza kila kitu kwenye maelezo yako ya polisi, unaweza kufafanua?” Shahidi akajibu, “Nilichoandika polisi ni summary, na katika summary huwezi kuandika kila kitu. Hiyo ndiyo sababu kwamba sijaandika kila kitu.”
Baada ya majibu hayo upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Renatus Mkude ulisema baada ya kumaliza ushahidi wa shahidi huyo, unakwenda kutafakari maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu juu ya mapingamizi mawili ambayo yaliletwa na mshtakiwa kuhusiana na vielelezo ambavyo Mahakama imevikataa.
Shauri hilo limeahirishwa mpaka kesho Oktoba 24, 2025 ambapo upande wa Jamhuri unatarajia kuleta shahidi wa nne.
Lissu anakabiliwa na shtaka la Uhaini linalodaiwa kuwa limetokana na maneno aliyoyazungumza kwenye hotuba yake ya Aprili 3,2025. Katika hotuba hiyo Lissu anadaiwa kuitisha Serikali na kuweka nia ya kufanya Uhaini