Kesi ya afande anayedaiwa kuwatuma vijana kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam, Fatma Kigondo inakuja leo baada ya mahakama kutoa hati ya wito kwa mara nyingine Agosti 23 mwaka huu.
Kesi hiyo ambayo imefunguliwa na Wakili Paul Kisabo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ilishindwa kuendelea kwa hatua ya usikilizwaji kutokana na afande huyo kutofika Mahakamani Agosti 23,2024.
Uamuzi wa kutolewa kwa hati nyingine ya wito ulitolewa na Hakimu Mkazi Dodoma Fransic Kishenyi ambaye anasikiliza kesi hiyo namba 23627 ya mwaka 2024.
Awali wakili anayemuakilisha Kisabo katika kesi hiyo Peter Madeleka aliiomba Mahakama kutoa utaratibu mwingine wa kumkamata kwa kutoa amri kwa kuwa afande huyo alipata wito wa kuitwa Mahakamani Agosti 22 lakini hakutokea.
Afande huyo ndiye anadaiwa kutajwa kwenye video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonyesha vijana watano wanaodai kutumwa na afande kumbaka na kumuingilia kinyume na maumbile binti wa 17 Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam.
Tayari washtakiwa wanne wamefunguliwa kesi ya ubakaji kwa kundi na kumuingilia kinyume na maumbile binti huyo ambapo kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma mbele ya Hakimu Mkazi, Zabibu Mpangule.
Washtakiwa hao ni Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), MT. 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, Askari Magereza C1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson, maarufu Machuche na Amini Lema maarufu Kindamba.