Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP Theopista Mallya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi.
Uhamisho wa RPC Mallya umekuja saa chache baada ya kauli yake juu ya binti aleyebakwa na kulawitiwa na vijana watano wanaodaiwa kutumwa na afande kufanya tukio hilo.
Katika mazungumzo yake na moja ya chombo cha habari RPC Mallya alinukuliwa kuwa
“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza”
-Mismamo wa Polisi-
Jeshi la Polisi Tanzania limesema kauli aliyoitoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya kuhusu binti aliyefanyiwa ukatili kuwa ‘alikuwa kama anajiuza’ si msimamo wa Jeshi hilo.
Hii ni baada ya RPC huyo kuzungumza na chombo kimoja cha habari nchini Tanzania kwa njia ya simu ambapo aliulizwa ikiwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na swali lingine aliloulizwa ni madai ya binti huyo kujiuza ambapo majibu ya kamanda huyo alisema hata kama ni hivyo hangestahili kutendewa hivyo.
“Jeshi la Polisi lingependa kuomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya Habari wakati ufuatiliaji ukifanyika kupata usahihi wake,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.
Kauli hiyo imezua gumzo mtandaoni kiasi wengi kukosa imani na Jeshi Ia Polisi wakiona kwamba haki ya msichana huyo inaminywa.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni kulisambaa video ikionyesha vijana watano wakidaiwa kumbaka na kumuingilia kinyume na maumbile binti anayedaiwa kuishi Yombo, Dar es Salaam, huku wakimtaka kumuomba afande samahani.
-Waziri Gwajima atia neno-
Kufuatia kauli hizo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, Dr. Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuwa watulivu, huku akiahidi haki kutendeka kwa binti aliyebakwa na kulawitiwa.
Msingi wa Kauli ya Dr. Gwajima umetokana na kauli ya RPC Mallya aliyoitoa jana Agosti 18,2024 alipozungumza na moja ya chombo cha habari nchini.
“Ndugu Wananchi, nimepokea ‘Tags’ nyingi za maoni na maswali kuhusu taarifa iliyotolewa na RPC mkoa wa Dodoma juu ya mwenendo wa shauri la ‘Binti wa Yombo’ (reja taarifa za awali).
Ndugu Wananchi, nimepokea hisia zenu, maoni na maswali yenu ambayo mmeelekeza kwangu. Nimewasiliana na Mhe Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye tayari naye amepokea na anafanyia kazi hivyo, tumpe nafasi atatoa taarifa yake.
Ndugu Wananchi, ni dhahiri kuwa, alichofanyiwa ‘Binti wa Yombo’ ni kitu kibaya kisicho cha utu hivyo, anastahili haki yake kwa mapana yote.
Ndugu Wananchi, Nawasihi tujipe muda na kuamini kuwa, haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na itaonekana bayana na siyo vinginevyo” ameandika Waziri Gwajima kwenye ukurasa wake wa X zamani (Twitter)