Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemkuta na kesi ya kujibu mtangazaji wa Clouds FM, Mwemba Burton (35) maarufu Mwijaku anayekabiliwa na kesi ya kusambaza picha za utupu (ngono).
Uamuzi huo umetolewa jana Mei 5, 2022 na Hakimu Mkazi Rhoda Ngimilanga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya uamuzi.
Akisoma uamuzi huo, hakimu Ngimilanga amssema, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano na vielelezo vinne uliotolewa na upande wa mashtaka, ameona kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu, hivyo anatakiwa kujitetea.
Mshtakiwa Mwijaku amedai katika utetezi wake atakuwa na mashahidi watatu na atajitetea kwa kiapo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 10, 2022 ambapo Mwijaku ataanza kujitetea.
Katika kesi hiyo inadaiwa, kati ya Septemba 17, 2019 na Oktoba 2019 jijini Dar Es salaam Mwijaku kwa kutumia mtandao wa Whatsupp alisambaza picha za utupu mtandaoni.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza picha hizo, wakati akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.