Kesi ya Lissu kuendelea Oktoba 6 kwa hatua ya ushahidi

Kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, inatarajiwa kuendelea Oktoba 6, 2025 baada ya kusomewa shtaka lake na kulijibu leo katika Mahakama Kuu.

Leo kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo kuhusu mapingamizi aliyowasilisha Lissu, ambapo alipinga uhalali wa hati ya mashtaka na pia akakosoa maelezo ya mashahidi akidai yameandikwa kinyume cha sheria.

Awali, akitoa uamuzi wa mapingamizi hayo, Jaji Danstan Ndunguru alisema Mahakama, baada ya kuzingatia hoja za pande zote na marejeo ya sheria mbalimbali, imeona kwamba hoja zilizotolewa na mshtakiwa hazina mashiko.

Kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka, Jaji Ndunguru alisema hati hiyo haina mapungufu yoyote na imekidhi vigezo vya kisheria kwani imeeleza maelezo ya kosa kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 135 na 138 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Aidha, kuhusu hoja ya nia ya kutenda kosa la uhaini, Jaji Ndunguru alisema hilo ni suala la ushahidi utakaotolewa mahakamani. Kuhusu hati kurekebishwa, alisema hati iliyotumika Mahakama ya Kisutu ilikuwa ni ya mapendekezo, ambayo hutumika wakati wa Committal. Baada ya taratibu kukamilika, hati hiyo hupelekwa Mahakama Kuu na ndiyo inayotumika katika kesi ya msingi baada ya DPP kujiridhisha.

Pia, kuhusu hoja ya kwamba maelezo ya mashahidi ni batili kwa sababu yanakiuka amri ya Mahakama Kuu ya kuwalinda mashahidi wa Jamhuri na kwamba maelezo ya polisi yalichukuliwa kinyume cha sheria, Jaji Ndunguru alisema hoja hizo zinahusu mwenendo wa Mahakama ya Kabidhi, ambayo tayari ilishatoa uamuzi.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Ndunguru alihitimisha kwa kusema kifungu cha 135 na 138 vilivyotumika kuandaa hati ya mashtaka vimejitosheleza.

 

-Mahakama yakataa kurusha kesi mubashara-

Mbali na uamuzi huo, Jaji Ndunguru alitolea maamuzi kuhusu ombi la mshtakiwa kutaka kesi irushwe mubashara (live). Alisema kesi hiyo haitarushwa moja kwa moja kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri utaratibu wa kulinda mashahidi kama ilivyoamriwa awali na Mahakama.

Katika maombi yake, Lissu alitaka umma uone na kufuatilia kinachoendelea mahakamani akisisitiza kuwa “haki siyo tu itendeke bali ionekane.”

Akitangaza uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji watatu, Jaji Ndunguru alisema ingawa kesi za jinai husikilizwa kwa uwazi, hakuna kanuni za kisheria nchini zinazowezesha kurusha moja kwa moja mashauri ya aina hiyo. Mahakama pia ilieleza kuwa kutokana na kuwepo mashahidi wa siri, matangazo ya mubashara yangetishia mwenendo wa ushahidi na hata usalama wa mshtakiwa.

Hata hivyo, Mahakama imeeleza kuwa kesi itaendelea kwa usikilizwaji wa wazi, hivyo watu na waandishi wa habari wataendelea kuhudhuria.

-Asomewa maelezo ya mashtaka-

Akisomewa maelezo ya mashtaka na Wakili wa Serikali, Thawabu Issa, Lissu alikubaliana na baadhi ya taarifa binafsi zikiwemo majina yake na ushiriki wake katika Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na maneno aliyoyatamka ambayo ndiyo msingi wa shtaka la uhaini.

Hata hivyo, alikanusha kwamba aliitisha mkutano wa wanahabari kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka, na pia akakana kuchapisha taarifa alizoelezwa. Alisema yeye alizungumza tu, na kuhusu kuchapishwa kwa taarifa hizo hana ufahamu wowote.

Upande wa Jamhuri umetangaza kuleta mashahidi 30, wakiwemo mashahidi wa siri, huku Lissu ambaye anajitetea mwenyewe akitarajia kuleta mashahidi 15, ambao wote amewataja wazi.

Miongoni mwa mashahidi aliowataja Lissu ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, IGP Camilius Wambura, Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, na Mkurugenzi wa Usalama na Ujasusi. Wengine ni Kamishna wa Polisi Ramadhan Ng’anzi, Agatha Atuhaire (Mwanaharakati kutoka Uganda), Boniface Mwangi na Martha Karua (Kenya), pamoja na Dk. William Mutunga, Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya.

Mashahidi wa Chadema aliowataja ni pamoja na John Heche (Makamu Mwenyekiti), John Mnyika (Kaimu Katibu Mkuu), Amani Sam Goligwa (Naibu Katibu Mkuu) na John Marwa (Mkurugenzi wa Jambo TV).

-Kukamatwa kwake-

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 mkoani Ruvuma, Wilaya ya Mbinga, muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara alipokuwa akinadi msimamo wa chama chake wa “No Reforms, No Election.”

Msimamo huo wa kisera uliopitishwa na Kamati Kuu ya CHADEMA Desemba 2–3, 2024, unadai kuwa chama hicho hakitashiriki Uchaguzi Mkuu iwapo hakutakuwa na marekebisho ya kimfumo, ikiwemo katiba mpya, marekebisho ya sheria, na uwepo wa tume huru ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Lissu na chama hicho, iwapo mabadiliko hayo hayatatekelezwa, basi uchaguzi hautafanyika nchini mwaka huu.