Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi mbili zinazomkabili, zikiwemo za uhaini na uchochezi.
Hata hivyo, mashauri hayo yamesimama kwa sasa, yakisubiri maamuzi muhimu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mahakama Kuu ya Tanzania.
-KESI YA UHAINI –
Kesi ya Lissu ngoma nzito, maamuzi ya DPP, na Mahakama Kuu yasubiriwa
Maombi hayo yaliwasilishwa kwa mujibu wa kifungu cha 262(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (kama kilivyofanyiwa marekebisho). Hata hivyo, Tundu Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, alipinga vikali ombi hilo akisisitiza kuwa hakuna sababu halali ya kuendelea kuahirisha kesi hiyo.
“Upande wa mashtaka umedai tangu awali kuwa upelelezi umekamilika na jalada liko kwa DPP. Ikiwa hakuna ushahidi wa kutosha, basi ni vema shauri hili liondolewe na mimi niachiliwe huru,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa ni takribani siku 90 zimepita tangu aliposomewa mashtaka na bado hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa na upande wa mashtaka, jambo alilolitafsiri kuwa ni uzembe na kutokuwepo kwa dhamira ya dhati ya kuendesha kesi hiyo.
Katika majibu yao, mawakili wa Serikali walisema hatua ya kusubiri uamuzi wa DPP inalenga kuhakikisha haki kwa mshtakiwa na kwamba jalada la shauri bado liko katika mchakato wa uamuzi wa mwisho.
Jaji Kiswaga alikubaliana na hoja ya Lissu kuwa Mahakama haiwezi kuendelea kuahirisha kesi bila sababu ya msingi, lakini alieleza kuwa hakuna sheria inayoelekeza kutoa amri ya kumlazimisha DPP kufuta au kupeleka kesi Mahakma Kuu.
“Ni kweli hoja za mshtakiwa zinaeleweka lakini sijaona sheria inayoelekeza kutoa amri kwa Jamhuri kumlazimisha DPP kututa au kupeleka kesi Mahakama Kuu” amesema Jaji Kiswaga.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama imeelekeza upande wa mashtaka kukamilisha taratibu zinazohitajika haraka ili kesi iweze kuendelea. Shauri hilo sasa limepangwa kusikilizwa tena Julai 15, 2025.
-KESI YA UPELELEZI-
Kwa upande mwingine, kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu imeshindwa kuendelea leo kufuatia pingamizi lililowasilishwa Mahakama Kuu na mawakili wa utetezi. Utetezi unapinga matumizi ya ushahidi wa siri uliopendekezwa na upande wa Jamhuri katika usikilizwaji wa shauri hilo.
Kwa sasa, Mahakama ya Kisutu imesubiri uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya uhalali wa ushahidi wa siri kabla ya kuendelea na hatua nyingine. Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa Julai 11, 2025.