Kesi ya Lissu yaahirishwa kufuatia kifo cha Msajili wa Mahakama Kuu

Kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa wa upinzani na Wakili wa kujitegemea, Tundu Antiphas Lissu imeendelea leo Oktoba 15 katika Mahakama Kuu masijala ndogo ya Dar es Salaam, ambapo aliendelea kumuhoji shahidi wa upande wa mashtaka, John Kahaya, kuhusu ushahidi unaohusiana na video ya mkutano wake wa tarehe 3 Aprili 2025.

Kesi hiyo, ambayo leo inachukua siku ya saba tangu ianze kusikilizwa kwa hatua ushahidi imekuwa ikivuta hisia za wananchi na wadau wa sheria, ilianza kusikilizwa majira ya saa tatu asubuhi ambapo Kahaya alianza kutoa ushahidi wake, na leo aliendelea kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa Lissu.

Kabla ya kuanza mahojiano, upande wa Jamhuri uliomba ruhusa kwa Mahakama kutokana na kuhudhuria msiba wa mtumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga ambaye ni Msajili wa Mahakama Asha Hamis Mwetindwa.

Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude aliieleza kuwa kutokana na dhehebu la Marehemu kwamba Muislam mwili utazikwa leo saa saba mchana, hivyo waliomba kesi iendelee kwa muda mfupi kabla ya kuahirishwa ili kutoa nafasi kwao kuhudhuria mazishi hayo.

“Waheshimiwa Majaji, juzi baada ya kuahirisha shauri hili tulipokea taarifa ya msiba wa mtumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga. Kwa mujibu wa taratibu, tumekuwa tukishirikiana katika matukio kama haya. Kwa kuwa ni haki ya mshtakiwa kesi iendelee, tunaomba mahojiano yaendelee hadi saa tano kabla ya kuahirisha,” alisema wakili Mkude.

Baada ya hatua hiyo, Lissu alianza kumuhoji Kahaya kwa kina kuhusu video inayodaiwa kuwa sehemu ya ushahidi muhimu katika mashtaka yanayomkabili. Alitaka kufahamu kama shahidi alikuwa amepata nafasi ya kuangalia tena video hiyo baada ya shauri hilo kuahirishwa wiki iliyopita.

Lissu: Baada ya yote niliyokuuliza siku ya Jumatatu, ulipata muda wa kuangalia tena ile video ya tarehe 3 Aprili 2025 ambayo wewe unasema uliiona Aprili 4,2025?

Shahidi:Hapana.

Lissu:Naomba uieleze Mahakama kama unajua video hiyo ilipelekwa kwenye mitandao ya Arusha One Digital, Mwanzo TV, Chanzo TV na Jambo TV X.

Shahidi:Sijapata

Lissu:Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba kusambaza au kusaidia kusambaza maandiko au taarifa zinazohusu uhaini nalo ni kosa la uhaini.

Shahidi:Sifahamu.

Katika kuendeleza hoja zake, Lissu alihoji iwapo shahidi anajua kwamba kutoa kauli pekee hakuwezi kuwa kosa la uhaini kwa mujibu wa sheria.

“Naomba uwaeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba kutoa kauli tu haliwezi kuwa kosa la uhaini kwa mujibu wa sheria zetu,” alisema Lissu. Shahidi akajibu, “Sifahamu.” Lissu akaendelea: “Ni kweli au si kweli kwamba ili kosa liwe la uhaini kwanza lazima kuwe na nia ya kutenda huo uhaini?” Shahidi akasema, “Kweli.” “Na ni kweli kwamba hiyo nia lazima ithibitishwe ama kwa maandishi au kwa matendo?” aliuliza tena Lissu, na shahidi akajibu, “Kweli.”

Baada ya hapo, Lissu alihoji kuhusu video hiyo yenyewe.

Lissu:Ni kweli au si kweli kwamba video ya tarehe 3 Aprili ilichapishwa kwenye mitandao kama Jambo TV na mingineyo?

Shahidi: Aliyechapisha sifahamu.

Lissu:Ni kweli au si kweli kwamba mkutano wangu wa tarehe 3 Aprili ulirushwa mubashara na Jambo TV?

Shahidi: Kweli

Lissu: Na ni kweli kwamba mimi (Lissu) si mfanyakazi wa Jambo TV na sina uhusiano wowote na Jambo TV?

Shahidi:Sikufanya upelelezi wa wahusika wa Jambo TV.

Lissu aliendelea kumkumbusha maneno aliyoyasema shahidi kwenye maelezo ya awali wakati wa ushahidi wake alipokuwa akiulizwa na upande wa Jamhuri

Lissu: Uliulizwa na Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema kama unaweza kuitambua ile video na maudhui yake, ukasema unaweza kuitambua, na ukasema mimi( Tundu Lissu)nimevaa kombati na nyuma kulikuwa na bendera.

Shahidi:Ndiyo.

Lissu: Sasa hayo maneno uliyaandika kwenye maelezo yako ya polisi siku tatu baadae baada ya kuiona hiyo video?” Shahidi:Sikuandika.

Lissu:Umezumgumza sana juu ya hiyo video, ukawaonyesha wakubwa zako, ukamuonyesha SSP George Bagemu, ukaipakua, sasa naomba uwaeleze Waheshimiwa Majaji kama hiyo flash uliiwasilisha Mahakamani.

Shahidi:Bado sijaiwasilisha.

Lissu:Kwa hiyo ni sahihi nikisema hakuna mtu aliyeiona isipokuwa wewe, Majaji hawajaiona wala mawakili wa Serikali hawajaiona?

Shahidi:Kweli

Lissu aliendelea kumhoji kwa hoja za kisheria, akimkumbusha kuwa amesoma sheria na hivyo anapaswa kujua Katiba ya nchi. “Waeleze Waheshimiwa Majaji, kwa ufahamu wako wa Katiba, kama kuna utaratibu umeandikwa wa namna ya kuzuia uchaguzi.” Shahidi akajibu, “Upo.” Lissu akamkazia: “Sasa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu unaendeshwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi?” Shahidi akasema, “Kweli.” “Na ni kweli kwamba Tume hiyo ni chombo huru kisichotakiwa kuingiliwa na mamlaka yoyote?” Lissu akauliza, naye shahidi akasema, “Sikumbuki.” “Waeleze kama Serikali ya nchi hii inaendesha uchaguzi mkuu,” aliuliza tena. “Kweli,” alisema shahidi.

-Hoja kuhusu mashtaka yenyewe-

Lissu alihoji zaidi kuhusu mashitaka yenyewe ambayo yanamkabili akigusia maneno aliyoyazungumza katika hotuba ambayo ndio imemuweka kizuizini hivi sasa

Lissu:Na mimi mashtaka yanayonikabili yanasema nilitaka kuhamasisha watu wazuie uchaguzi mkuu wa 2025, ni kweli au si kweli?

Shahidi:Inategemea.

Lissu:Umeiangalia vizuri hiyo hati ya mashtaka?

Shahidi:Sijaiangalia.

Lissu akaendelea kumkazia hoja: “Kwa hiyo hujui nashtakiwa kwa nini?” Shahidi hakujibu, na Lissu akaendelea kumuuliza maswali mengine.

Katika hatua nyingine, Lissu alimkumbusha shahidi kwamba katika maneno aliyoyasema hakuna hata neno moja alilotaja Serikali.

Lissu:Kwenye hayo maneno niliyoyasema hakuna neno hata moja nimetaja Serikali, ni kweli au si kweli?

Shahidi:Serikali ipo.

Lissu akaendelea, Shahidi, kwenye visomo vyako ulisoma sheria za jinai?”

Shahidi akasema, “Kweli.” “Na umesoma pia sheria yetu kuu ya jinai?” Shahidi akajibu , “Nimesoma.”

Lissu: Mimi nimeshtakiwa kwa kosa la Uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d), sasa waeleze Waheshimiwa Majaji kama katika kifungu hicho neno ‘kutishia’ limefafanuliwa,” aliuliza Lissu.

Shahidi: Sikumbuki, alijibu shahidi. “Nikikuambia kwamba hilo neno ‘kutishia’ halijafafanuliwa mahali popote kwenye Penal Code, utasemaje?” Lissu akaendelea. “Sifahamu,” alisema shahidi.

Katika uendelezaji wa mahojiano hayo, Lissu alimuuliza: “Maneno ya majaji ni wa CCM niliyoyazungumza, je hayo ni ya kihaini?” Shahidi akajibu, “Hakuna sehemu wanasema ni ya kihaini.”

Tundu Lissu alikamatwa Aprili 9, 2024, mkoani Ruvuma na kupelekwa Dar es Salaam. Siku iliyofuata, Aprili 10, 2024, alishitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Anakabiliwa na shitaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, kilichotokana na maneno aliyoyatamka yanayohusiana na mpango wa kudhibiti au kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025.

Mashitaka haya yamevutia umakini mkubwa wa umma na vyombo vya habari, huku wananchi wengi wakisubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama Kuu

Kuachiwa huru au kuendelea kusota rumande, jambo linaloangaliwa kuwa na athari kubwa kisiasa na kisheria nchini Tanzania.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho mapema asubuhi kwa ajili ya Lissu kuendelea kumuhoji Shahidi maswali ya Dodoso