Kesi ya Lissu:Hatima ya vielelezo vya video kesi ya Lissu kujulikana Jumatano

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, imeendelea leo Oktoba 20,2025, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo pande zote zimewasilisha hoja nzito kuhusu kupokelewa kwa vielelezo vya video na vifaa vya kielektroniki vilivyotolewa na upande wa mashtaka.

Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe, anakabiliwa na shtaka la uhaini yanayodaiwa kutokana na matamshi aliyotoa Aprili 3,2025. Alikamatwa Aprili 9, 2025 mkoani Ruvuma na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam, ambako anakabiliwa na kesi hiyo mbele ya jopo la majaji wa Mahakama Kuu.

Anadaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, ulijibu pingamizi za Lissu lenye hoja nne,  aliyepinga Mahakama kupokea vielelezo vya video, flash disc na memory card zilizowasilishwa na shahidi wa tatu wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi Samweli Kaaya (39) kutoka Kitengo cha Picha, Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai Makao Makuu Dar es Salaam.

Shahidi Kaaya alieleza mahakamani jinsi alivyofanya uchunguzi wa picha mjongeo (video) na kubaini kuwa hazikutengenezwa wala kubadilishwa. Pia aliomba kutumia flash disc na memory card kuthibitisha kuwa ni vifaa vilevile alivyofanyia kazi wakati wa uchunguzi wake, jambo lililoibua pingamizi kutoka kwa Lissu.

Katuga alisema hoja ya Lissu kwamba vielelezo hivyo havikusomwa wakati wa hatua ya awali ya kesi (comital) haina msingi, akibainisha kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria ya Ushahidi wa Kielektroniki ya mwaka 2023 sura ya 6, ushahidi wa kielektroniki kama video unachukuliwa kama nyaraka za kisheria. 

“Video hizi ziko katika mfumo wa kielektroniki na kwa tafsiri ya sheria ni nyaraka. Kwa hiyo, hazihitaji kusomwa upya kama vielelezo vya kawaida,” alisema Katuga.

Akiendelea kujibu hoja za Lissu, Katuga alisema hakuna kifungu cha sheria kinacholazimisha kwamba shahidi wa kitaalam atoe ripoti kwanza kabla ya vielelezo, akisisitiza kuwa mpangilio wa ushahidi hutegemea mazingira ya kesi. Kuhusu hoja ya mnyororo wa utunzaji wa vielelezo (chain of custody), alisema si lazima uthibitishwe na shahidi mmoja, na kwamba maelezo ya Jamhuri yanaonyesha vielelezo hivyo vimehifadhiwa kwa usahihi.

Baada ya Serikali kumaliza hoja zake, Lissu alijibu moja kwa moja akisema kuwa video hizo hazijawahi kuchezwa katika Mahakama ya Kisutu wakati wa hatua ya awali ya kesi, hivyo haziwezi kuletwa sasa kama vielelezo vipya. 

“Mashauri ya Kisutu yalikuwa ya wazi, hayakufanyika kwa kificho. Wala video hizi hazikuonyeshwa. Ni kweli ziliandikwa kwenye orodha ya vielelezo, lakini hazikuchezwa hadharani,” alisema Lissu.

Akiendelea, Lissu alipinga hoja ya Serikali kwamba hakuna ulazima wa kuanza na ripoti ya kitaalam kabla ya vielelezo, akisema ushahidi wa kitaalam lazima uanzie na ripoti ya mtaalam aliyehusika. 

“Haiwezekani shahidi aseme ameandika ripoti halafu haiwasilishwi. Vifungu vyote nilivyovitaja vinazungumzia ripoti ya mtaalam ndiyo msingi wa ushahidi wa kitaalam,” alisisitiza.

Kuhusu hoja ya tatu inayohusu uwezo wa shahidi (competence), Lissu alisema shahidi wa kitaalam hawezi kutambulika kwa maelezo yake ya mdomo pekee bali lazima ateuliwe rasmi na Mkurugenzi wa Mashtaka na uteuzi wake kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali. “Kama hajateuliwa, maneno yake ni kazi bure,” alisema Lissu.

Katika hoja yake ya mwisho, Lissu alisisitiza kuwa mnyororo wa utunzaji wa vielelezo umevunjika na kwamba Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kuwa flash disc na memory card ni zilezile zilizofanyiwa uchunguzi.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.

Kesi  imeahirishwa hadi Oktoba 22, 2025 saa tatu asubuhi, kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusu iwapo vielelezo vya video na vifaa vya kielektroniki vitakubaliwa kama sehemu ya ushahidi au la.