Kesi ya Maofisa wa Polisi yapigwa kalenda

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara leo imeahirisha kesi ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa polisi mkoani Mtwara hadi Februari 22, 2022 itakapotajwa tena.

Akiahirisha kesi hiyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Lugano Kasebele amesema anaahirisha kesi hiyo kutokana na upelelezi kutokamilika.

Washtakiwa wanaohusishwa na mauaji hayo ni ofisa Upelelezi (OC CID) Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara (OCS), Charles Onyango, Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya pamoja na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi, Marco Mbuta. Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 25 na kusomewa shitaka la mauaji ya kukusudia.

Inadaiwa kuwa Januari 5 mwaka huu maofisa hao wa polisi walimuua Musa Hamis (25), mkazi wa Nachingwea mkoani baada ya kumpora shilingi  milioni 70. 

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 3.12 asubuhi chini ya ulinzi mkali licha ya kuwa wanahabari walizuiwa kuingia ndani ya chumba cha Mahakama

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja George kwa niaba ya Jamhuri amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

Hakimu Kasebele amesema kuwa kwa vile upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo ameahirisha kesi hadi Februari 22, 2022 itakapotajwa tena.