Jopo la Mawakili wa utetezi 14 limejitokeza kuwatetea washtakiwa 25 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya askari mmoja katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro.
Askari huyo aliuawa Juni 10, 2022 baada ya kushambuliwa kwa kupigwa mshale na kundi la watu wenye silaha wakati wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka.
Leo Juni 30, 2022 watuhumiwa hao wakiwemo madiwani tisa wa wilaya hiyo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo Ndirango Laizer walifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Mbele ya Hakimu Mkazi Herieth Mhenga, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Upendo Shemkole huku utetezi wakiongozwa na Wakili Jeremia Mtobesya.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba 11/2022 mawakili wengine wa utetezi ni Jebra Kambole, Joseph Ole Shangai, Peter Madeleka, Denis Mosses, Adolf Temba, William Ernest, Yonas Masiaya, Nicholous Ole Senteu, Samaito Mollel, Julius Lukumay, Ngeeyan Laizer, Deogratias Njau na John Lairumbe.
Wakili Upendo aliieleza mahakama kuwa shauri hilo limepangwa kwa ajili ya kutajwa ila wanaomba kubadilisha hati ya mashtaka ili waongeze shitaka moja.
Kutokana na ombi hilo mawakili wa utetezi waliwasilisha pingamizi ambapo Wakili Mtobesya na Madeleka walipinga ombi hilo na kueleza mahakama kuwa ombi hilo limekuja kwa hatua ambayo siyo stahiki.
“Ni wazi hii kesi ipo kwenye hatua za mwanzoni, kwa namna yoyote kubadilisha hati ya mashitaka ni kinyume na matakwa ya kisheria kwani mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, tunaomba mahakama ikatae maombi ya Jamhuri kurekebisha hati ya mashtaka,” amesema Madeleka
Akijibu hoja hiyo Wakili Upendo alidai mahakamani hapo kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza na kesi hiyo ipo kwenye hatua za upelelezi na kuwa walichowasilisha mahakamani hapo ni kubadili hati na kuongeza kosa na kimsingi sheria haizuii mahali popote kubadili hati ya mashitaka.
Baada ya hoja hizo mahakama iliahirisha kwa muda kesi hiyo na ilirejea kwa ajili ya uamuzi mdogo ambapo Hakimu huyo alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama inaruhusu kubadilisha hati hiyo ya mashtaka na kuwa hakuondoi haki yoyote ya washitakiwa hao.
“Kuruhusu kubadilisha hati ya mashitaka hakuondoi haki yoyote kwa washitakiwa na hakuna sheria yoyote inayokataza hati ya mashitaka kubadilisha hati ya mashitaka,”
Akiwasomea hati hiyo mpya ya mashitaka, Wakili Upendo alidai kosa la kwanza ni njama ya mauaji, ambapo kwa tarehe na sehemu isiyofahamika Ngorongoro, walipanga njama ya kuua maofisa wa Serikali na maofisa wa Polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.
Amedai kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10,2022 eneo la Ololosokwan wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo cha G 4200 Koplo Garlus Mwita.
Wakili Mtobesya aliomba upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwani baadhi ya washitakiwa hao umri umeenda huku mmoja akiwa ni mwanafunzi, ili waweze kupata haki yao ya kusikilizwa.
Hakimu huyo aliwataka washitakiwa hao kutokujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo na kesi hiyo kuahirishwa hadi Julai 14, 2022 itakapotajwa tena.