Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini  inayowakabili Maafisa saba wa polisi yaanza kusikilizwa

Kesi ya mauaji inayowakabili Maafisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara imeanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara.

Maofisa hao wamepanda kizimbani leo Agosti 9 kusikiliza shauri la kesi hiyo wakidaiwa kutenda mauaji ya Mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis (25) mkazi wa Nachingwea mkoani Mtwara.

Wanaoshitakiwa ni Mrakibu wa polisi na Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mrakibu msaidizi wa polisi, aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi Mtwara, Charles Onyango, Mrakibu wa polisi, aliyekuwa Mkuu wa intelijensia Mkoa, Nicholaus Kisinza, Mkaguzi wa polisi, John Msuya, Mkaguzi msaidizi wa polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa polisi, Shirazi Ally Mkupa na askari na G5158 Kopro Salum Juma Mbalu.

Kesi hiyo namba 15 ya mwaka 2023 inaongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahaka hiyo Rose Ebrahim, ilianza kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara Mei 4. Ilihamishwa kwenye Mahakama Kuu ya Kanda ya Mtwara kutokana na mahakama hiyo ya mwanzo kutokuwa na hadhi ya kusikiliza.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la mawakili wanne kutoka upande wa Serikali na 10 wa upande wa washtakiwa.

Maafisa saba wa polisi walifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakamani hapo Januari 2022 kwa shitaka la mauaji ya Mfanyabiashara wa madini, Musa Hamis Hamis ( 25), Mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea Mkoani Lindi.

Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Januari 5, 2022 mkoani hapa.

https://mwanzotv.com/2022/02/22/kesi-ya-maofisa-saba-wa-polisi-wanaodaiwa-kuua-yapigwa-tena-kalenda/