Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Jumatano Oktoba 20, 2021 imetupilia mbali mapingamizi yote yaliyowekwa na upande wa utetezi waliotaka Mahakama isipokee maelezo ya mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa kwa madai yalitolewa nje ya muda wa kisheria na mtuhumiwa alitishiwa kuteswa.
Akisoma uamuzi huo wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi namba 16 ya 2021, kesi ya Uhujumu Uchumi yenye makosa ya ugaidi ndani yake, Jaji Mustapha Siyani amesema kwamba mapingamizi hayo yamekosa mashiko ya kisheria na kwamba maelezo ya mshtakiwa yalichukuliwa ndani ya muda.
Kwa mujibu wa sheria mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi anatakiwa kuhojiwa na kuchukuliwa maelezo ndani ya saa 4 tangu alipokamatwa na hii imebainishwa katika kifungu cha sheria namba 50 kifungu kidogo cha 1(a) na (b) na kifungu cha 51 na 52 sura ya 20 ya sheria inayoongoza makosa ya jinai.
Katika pingamizi la kwanza upande wa utetezi ulipinga maelezo ya onyo yaliyoandikwa nje ya muda na mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa.
Katika uamuzi wa jaji Siyani ametupilia mbali pingamizi hilo ambapo ameeleza kuwa anakubaliana na Jamhuri kuwa mazingira yaliyokuwepo yana mantiki kuwa walikuwa wakiendelea na upelelezi.
Amesema kuchelewa kuhojiwa kwake kulikuwa na sababu za kisheria chini ya kifungu cha 51(1) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Katika pingamizi la pili mahakama imekataa hoja ya pili kuwa Adamu Kasekwa aliteswa kwani hakutatolewa ushahidi huo. Hivyo maelezo yalitolewa na mshtakiwa wa pili kwa ridhaa yake.
Mara baada ya uamuzi huo kutolewa hii inapisha nafasi ya shauri la msingi kuendelea, lilipoishia, lakini kabla ya kuendelea kwa shauri hilo jaji Siyani anajiondoa kuendelea kusikiliza shauri hilo kutokana na majukumu mengi aliyokuwa nayo.
Siyani hivi karibuni aliteuliwa na Rais Samia Suluhu kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania.