Kesi Ya Mbowe: Jaji adai mapingamizi yaliyoletwa na utetezi hayana mashiko

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Jumatano Oktoba 20, 2021 imetupilia mbali mapingamizi yote yaliyowekwa na upande wa utetezi waliotaka Mahakama isipokee maelezo ya mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa kwa madai yalitolewa nje ya muda wa kisheria na mtuhumiwa alitishiwa kuteswa.

Akisoma uamuzi  huo wa kesi  ndogo ndani ya kesi ya msingi namba 16 ya 2021, kesi ya Uhujumu Uchumi yenye makosa ya ugaidi ndani yake, Jaji Mustapha Siyani amesema kwamba mapingamizi hayo yamekosa mashiko ya kisheria na kwamba maelezo ya mshtakiwa yalichukuliwa ndani ya muda.

Kwa mujibu wa sheria mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi anatakiwa kuhojiwa na kuchukuliwa maelezo ndani ya saa 4 tangu alipokamatwa na hii imebainishwa katika kifungu cha sheria namba 50 kifungu kidogo cha 1(a) na (b) na kifungu cha 51 na 52 sura ya 20  ya sheria inayoongoza makosa ya jinai.

Katika pingamizi  la kwanza upande wa utetezi ulipinga maelezo ya onyo yaliyoandikwa nje ya muda na mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa.

Katika uamuzi wa jaji Siyani ametupilia mbali pingamizi hilo ambapo ameeleza kuwa anakubaliana na Jamhuri kuwa mazingira yaliyokuwepo yana mantiki kuwa walikuwa wakiendelea na upelelezi.

Amesema kuchelewa kuhojiwa kwake kulikuwa na sababu za kisheria chini ya kifungu cha 51(1) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Katika pingamizi la pili mahakama imekataa hoja ya pili kuwa Adamu Kasekwa aliteswa kwani hakutatolewa ushahidi huo. Hivyo maelezo yalitolewa na mshtakiwa wa pili kwa ridhaa yake.

Mara baada ya uamuzi huo kutolewa hii inapisha nafasi ya shauri la msingi kuendelea, lilipoishia, lakini kabla ya kuendelea kwa shauri hilo jaji Siyani anajiondoa kuendelea kusikiliza shauri hilo kutokana na majukumu mengi aliyokuwa nayo.

Siyani hivi karibuni aliteuliwa na Rais Samia Suluhu kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania.

Askofu wa Kanisa  Emmaus Mwamakula wa kanisa la Uamsho la Moravian, akiaongoza mawakili wa utetezi kabla kutolewa uamuzi wa kesi ndogo mahakamani 20 Oktoba.


Nje ya mahakama Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika anasema hawajaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na jaji Siyani katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa na kwamba kesi hii inatumika kama shambulio la kisiasa.
 
“Uamuzi mdogo uliotolewa na Jaji leo hatujaridhika nao, Uamuzi katika mapingamizi yote mawili. Jaji ambaye kwa sasa ni Jaji Kiongozi hajaonyesha uongozi wa kutenda haki. Tutakwenda kukutana kama chama kutafakari kwa kina wakati Mawakili wakishauriana na Watuhumiwa.” amesema Mnyika
 
Pamoja na hayo Mnyika amewataka wanachama wa chama hicho kuwa wawewastahimilivu huku akisisitiza kwamba suala la kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi linapaswa kuendelea.
 
Katibu Mkuu huyo wa Chadema amedai, maamuzi ya mahakama hiyo dhidi ya mapingamizi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi katika kesi hiyo, yatatumika katika Mahakama ya Rufaa, kama hoja za utetezi endapo Mahakama hiyo ya Uhujumu uchumi itamkuta na hatia Mbowe.
Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, akizungumza na wanahabari nje ya Mahakama

Mnyika amesema, Chadema itatumia njia nyingine kutafuta uhuru wa Mbowe na wenzake.

“Tutaendelea na mapambano ya kutafuta haki kwenye mahakama hii, mapamabano yatendelea kwa jaji mwingine. Lakini tutatumia vilevile njia nyingine za kutafuta haki ili haki ipatikane kwa wakati,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Siku 92 za kukaa ndani na maelezo ya jaji anaonesha kesi itachukua miezi mingine miwili au mitatu, maana yake tunaingia kwenye kundi la haki kucheleweshwa. Kwa vyovyote vile lazima kila mpenda haki tuungane pamoja kudai haki ipatikane mapema.”