Kesi Ya Tundu Lissu Yaahirishwa Hadi Aprili 28

Kesi ya Uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu inatarajiwa kuitwa tena Aprili 28, 2025 huku kesi ya Uhaini ikipangwa kuitwa Mei 7, 2025.

Haya yamejiri leo baada ya siku ngumu ya mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa utetezi na mawakili wa Serikali, ambapo licha ya hapo awali Mahakama kuamuru Lissu kufikishwa leo kwa mara ya pili lakini, imekwenda tofauti baada ya Mawakili wa utetezi kuelezwa kua kesi hiyo itaendeshwa kwa njia ya Mtandao.

Hata hivyo Lissu alikataa kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya Mtandao na kueleza mawakili wake kwamba haogopi mashtaka aliyopewa bali anataka kesi hiyo iendeshwe kwa wazi ili kila mmoja apate kufatilia.

Akizungumza nje ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Wakili anayeoongoza jopo la Mawakili zaidi ya 20 linalomtetea Tundu Lissu, Dkt Rugemeleza Nshala ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ameshangazwa na namna ambavyo kesi hiyo imeendeshwa hii huku kukiwa na vikwazo kutoka vyombo vya dola na Mamlaka kwa kuzuia watu kuingia Mahakamani jambo linaloashiria uminywaji wa haki kwani hata wao pia kama Mawakili walinyimwa fursa ya kuonana na mteja wao.

Kufuatia hayo mawakili wa utetezi wameweka mapingamizi ya kesi hiyo kutoendeshwa kimtandao.

Nshala amesema yaliyoendelea leo yameonyesha mashaka juu ya kupata haki jinai. Kwa upande wake, Wakili Alute Mghwai ambaye pia ni ndugu wa Lissu, alieleza kuwa hali anayoishi Lissu akiwa gerezani ni kama tayari ameshahukumiwa, jambo linalokiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.