Kesi ya uhaini inayomkabili Lissu yaahirishwa hadi Mei 19, Mahakama yatoa onyo

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, imeahirishwa kwa siku 13 hadi Mei 19, 2025, baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa upelelezi haujakamilika.

Kesi hiyo, inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilipangwa kutajwa leo kwa njia ya mtandao. Hata hivyo, mshtakiwa Lissu aligoma kushiriki kwa njia hiyo, akisisitiza kutaka kufikishwa mahakamani moja kwa moja.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tawabu Yahaya, akiongoza jopo la mawakili wa Jamhuri, aliieleza Mahakama kuwa bado wanakamilisha taratibu za upelelezi, na hivyo kuomba ahirisho la muda zaidi. Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi waliotaka kufahamu ni lini hasa upelelezi utakamilika, wakieleza kuwa hati ya mashtaka inaonesha wazi tuhuma zinazomkabili Lissu.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Franco Kiswanga, alitoa wito kwa upande wa Jamhuri kuhakikisha wanakamilisha upelelezi kwa haraka. Alisisitiza kuwa katika tarehe ijayo, Mahakama inatarajia kupata taarifa sahihi kuhusu hatua ya upelelezi kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Katika hatua nyingine, Lissu ambaye anashikiliwa katika Gereza la Ukonga, alitangaza kuanza mgomo wa kula kuanzia leo ikiwa hatofikishwa mahakamani kama alivyoomba. 

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara mkoani Ruvuma. Alikuwa akiendelea kusambaza msimamo wa kisera wa CHADEMA unaojulikana kama *“No Reforms, No Election”* — msimamo uliopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho katika kikao chake cha Desemba 2–3, 2024.

Msimamo huo unasisitiza kuwa CHADEMA haitashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu iwapo hakutafanyika mabadiliko ya msingi ya kisheria na kikatiba, ikiwemo kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.