Kesi Ya Uhaini Ya Lissu- Shahidi: Kutoa Maudhui ya Uchochezi ni Uhaini

Shahidi katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ameieleza Mahakama kwamba maudhui yenye Uchochezi ni kosa la Uhaini.

Shahidi: Kutoa maudhui ya Uchochezi ni Uhaini

Ameeleza hayo leo Oktoba 7,2025 wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Mahakama akiongozwa kwa maswali ya dodoso aliyokuwa akiulizwa na mshtakiwa Tundu  Lissu ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo.

Shahidi huyo ambaye ni ACP George Bagemu, mwenye umri wa miaka 48, alisema kwamba kutoa maudhui ya Uchochezi ni kosa la Uhaini na ndilo ambalo anashtakiwa nalo mtuhumiwa.

Lissu: Waeleze majaji kwamba mtu anaetoa  maudhui ya Uchochezi ni kosa la Uhaini. Je maudhui yenye Uchochezi kwa umma ni kosa la Uhaini au sio

Shahidi :Ni kosa la Uhaini

Lissu: Hayo maudhui ya Uchochezi kwa umma yanaingia kwenye kifungu cha 39(2d), kifungu ambacho mmenishtakia kwa kosa la Uhaini.

Shahidi: Ndio yanaingia

Ushahidi huo ambao umeingia siku ya pili, pamoja na mambo mengine katika ushahidi wake ACP. Bagemu aliieleza Mahakama pia aliandika maelezo yake kwa siku mbili tofauti yaani tarehe 8 Aprili na tarehe 10 Aprili na kukubali maelezo yaliyopo Mahakamani hapo ni yake bila ubishi.

Lissu: Shahidi ACP George Bagemu ndio jina lako kamili
Shahid: Ndio jina langu

Lissu: Shahidi naomba uwaambie Waheshimiwa majaji kabla ya kuja kutoa ushahidi jana uliandika maelezo kama shahidi

Shahidi: Ndio niliandika maelezo kama shahidi

Lissu: Ni kwei uliandika maelezo mara mbili kwa maana tarehe 8 Aprili na ukaandika maelezo tarehe 10 Aprili

Shahidi: Ndio niliandika maelezo mara mbili, niliandika  na ya nyongeza.

Lissu: Naomba uwaeleze Waheshimiwa Majaji hizo karatasi mbili ulizoshikilia ni vitu gani?

Shahidi: Nikianza na karatasi ya mwanzo haya ni maelezo ya SSP George Bagemu na hii ya pili ni “scanned copy “ lakini ni maelekezo yangu niliyotoa tarehe 10 Aprili

Lissu: Waambie majaji kama hizo sahihi ni za kwako

Shahidi: Hizi sahihi ni za kwangu

Alikwenda mbali zaidi Shahidi huyo aliiambia Mahakama kwamba aliandika mwenyewe maelezo yake ushahidi licha ya sheria kumtaka kutoa maelezo akiwa na msimamizi.

Lissu: Waeleze majaji kuhusiana maelezo yako ya ushahidi uliandika na nani

Shahidi: Niliandika mwenyewe

Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji kabla ya kuandika maelezo hayo uliomba ushauri wa kisheria kwa mwanasheria yoyote

Shahidi: Sikuomba ushauri wowote

Lissu: Kwenye maelezo yako ulitaja kwamba umeyaandika chini ya kifungu cha 10(3) cha sheria ya mwenendo wa jinai

Shahidi: Kweli

Lissu: Ni kweli au si kweli kifungu hicho ambacho sasa hivi ni kifungu ch 11(4) hairuhusiwi kujiandikia maelezo mwenyewe

Shahidi: Hakuna sheria inayonizuia nisiandike maelezo yangu mwenyewe

Lissu: Nani aliyekukanya, kuandika maelezo maana huwa kuna mtu ndio anaekanya

Shahidi: Mimi mwenyewe

Lissu: Nani aliyethibitisha maelezo yako

Shahidi: Mimi mwenyewe.

Katika maelezo yake ACP Bagemu, amepitia hatua mbalimbali za kielimu ikiwamo kuchukua kozi fupi fupi hadi kufikia hatua yanayokupandishwa cheo alichonacho sasa. Kadhalika Shahidi aliulizwa uzoefu wake katika kusthaki watu maarufu kwenye kesi kubwa kama hii ya Uhaini, kwa iwapo kesi hizo zilimalizika kwa hatua ya  hukumu kwa maana ya mtuhumiwa kukutwa na hatia.

Lissu : Naomba uwaeleze Waheshimiwa majaji katika miaka yako 22 ya upolisi kama umewahi kufanya uchunguzi wa kesi zinazohusu kesi kubwa za kisiasa au zenye umuhimu wa umma kama  hii.

Shahidi: Niliwahi, ikiwemo ya Dk Slaa nyingine ilikua ya Lembeli kwangu mimi hii ni kesi ya tatu nakumbuka

Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji, katika miaka 22 ya upolisi wako uliwahi kufanya kazi kesi ngapi mtu muhimu kisiasa ameshtakiwa.

Shahidi: Kesi nne

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba hakuna kesi yoyote kwenye kesi kubwa kuna mtu aliyepatikana na hatia

Shahidi: Kweli

Lissu: Ni kweli hakuna kesi ambayo umechunguza wewe ambayo ilifika hatua ya hukumu

Shahidi: Kweli, ila ya Tundu Lissu itafika.

Kesi imeahirishwa mpaka kesho saa tatu asubuhi, ambapo Lissu ataendelea kumuhoji Shahidi maswali ya dodoso. Lissu ambaye leo anatimiza siku 182 gerezani anashtakiwa kwa kosa la Uhaini analodaiwa kulitenda mnamo Aprili 2025 kupitia mkutano wake na Wanahabari, ambapo kwa mujibu wa sheria za Tanzania kosa hilo hukumu ni kifo.