Kesi ya Uhaini inayomkabili Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antiphas Lissu, imeendelea leo katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, ambapo leo shahidi wa pili wa Jamhuri amemaliza kutoa ushahidi wake na kuruhusu shahidi watatu kuendelea kutoa ushahidi wake.
Katika kesi hiyo, Lissu anadaiwa kutoa maneno yenye nia ya kuitisha Serikali kwa kuhamasisha kuzuia uchaguzi Mkuu wa 2025 kupitia taarifa aliyoitoa Aprili 3,2025.
Awali leo kabla ya kuendelea na shahidi wa tatu mahakamani Lissu ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo alimalizia maswali ya dodoso ambayo kimsingi alizungumzia kuhusu picha mjongeo ama video ambayo abadaiwa kuochapisha.
Katika kuhojiana na shahidi huyo, Lissu alianza kwa kuuliza kama fomu namba PF145, ambayo ilielezwa kuwa ilisindikizwa na flash disk, ilisomwa wakati wa mchakato wa Committal katika Mahakama ya Kisutu. Hata hivyo, shahidi alijibu kuwa hakuwepo Kisutu wakati huo.
“Waeleze Waheshimiwa Majaji kama uliwasilisha hiyo fomu,” alihoji Lissu, ambapo shahidi alijibu kwa kifupi, “Sijaiwasilisha.”
Baada ya hapo, Lissu alihamishia hoja zake kwenye masuala ya uchaguzi, akimtaka shahidi kueleza kama anafahamu kuhusu kauli ya Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, aliyowahi kusema wagombea wa upinzani walioenguliwa wangerejeshwa endapo wangekata rufaa.
Hata hivyo, kwa kila swali lililohusu uamuzi wa Tume ya Uchaguzi, uamuzi wa mawaziri, au takwimu za uchaguzi wa mwaka 2020, shahidi alijibu kwa maneno yanayofanana Sikumbuki au Sifahamu.
Katika moja ya hoja zilizozua gumzo mahakamani, Lissu alihoji:
“Unafahamu kwamba kwenye uchaguzi ule asilimia 99 ya wenyeviti walikuwa ni wa CCM?”
Lakini shahidi alijibu, Sifahamu.
Lissu aliendelea kusisitiza kuwa mfumo wa uchaguzi nchini unadhibitiwa na wateule wa Rais, akitaja kuwa maafisa waandikishaji, makatibu tawala wa wilaya, na hata majaji wanaosimamia kesi za uchaguzi wote ni wateule wa Rais.
Shahidi alijibu, Ni kweli, lakini Rais anafanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote, si chama fulani.
Lissu hakusita kuhoji kuhusu ripoti za waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wa mwaka 2020 kutoka Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ulaya, na Jumuiya ya Madola, akitaka kufahamu kama shahidi alizisoma ripoti hizo ambazo zilipendekeza Tanzania ikamilishe mchakato wa Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mwingine.
Shahidi alijibu kwa utulivu, Sikuwahi kuzisoma.
-Mvutano Kuhusu Video ya Jambo TV-
Sehemu nyingine ya kesi hiyo ilihusu video ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha mashtaka dhidi ya Lissu.
Lissu alihoji kwa kina kuhusu chanzo cha video hiyo iliyochapishwa kwenye Jambo TV, akitaka kujua kama shahidi anafahamu ni nani aliyeiweka, kuisambaza, au kufanya “upload” kwenye mtandao wa YouTube.
Katika majibizano hayo, shahidi alidai, “Ni wewe kupitia Jambo TV” akimaanisha Lissu ndiye aliyesambaza
Lissu aliendelea kuhoji: Nani aliye na ‘password’ ya Jambo TV? Je, mimi nilikuwa na uwezo wa kuingia kwenye ‘platforms’ za Jambo TV kufanya hayo yote?
Shahidi: Sifahamu
Baada ya maswali kadhaa, Lissu alimaliza kumuhoji shahidi na kuileza Mahakama kwamba amefika mwisho wa maswali ya dodoso na shahidi huyo ambaye ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi John Kahaya.
Baada ya kumalizika kwa mahojiano ya Lissu, saa 10:18 asubuhi , upande wa mashtaka ulipata nafasi ya kufanya “re-examination” yaani maswali ya kusawazisha kwa lugha rahisi kupitia Wakili wa Serikali Nassoro Katuga.
Katika maswali yake, Katuga alimtaka shahidi kufafanua kuhusu tarehe ya kuajiriwa kwake Jeshini, akisema awali aliwahi kutamka miaka miwili tofauti — 2005 na 2006.
Shahidi alieleza kuwa mwaka 2005 aliteuliwa kuanza mafunzo ya Polisi, na mwaka 2006 ndio alihitimu rasmi na kuanza kazi.
Katuga pia alimuuliza kuhusu utofauti wa majibu aliyoyatoa Oktoba 15 kuhusu nani aliyechapisha video mtandaoni, ambapo awali alisema “sijui”, lakini leo alisema “ni Lissu kupitia Jambo TV.” Akifafanua, shahidi alisema:
“Waheshimiwa Majaji, mshtakiwa Tundu Antiphas Lissu alichapisha maudhui yaliyomo kwenye hati ya mashtaka. Kitendo cha yeye kuwaalika wanahabari wa Jambo TV kilikuwa tayari ni dhamira ya kusambaza maudhui hayo mtandaoni.”
Baada ya maelezo hayo, upande wa Jamhuri ulimaliza kumhoji shahidi wa pili, na Wakili Renatus Mkude alisimama kuwatambulisha mahakamani kuwa upande wa mashtaka ulikuwa tayari kumuita shahidi wa tatu, Mkaguzi wa Polisi, Samweli Eribariki Kahaya.
Kahaya, mwenye umri wa miaka 39, alijitambulisha kuwa ni Afisa wa Polisi katika Kitengo cha Picha cha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Thawabu Issa, shahidi huyo alieleza kuwa yeye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha na video za matukio ya uhalifu, baada ya kuteuliwa rasmi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kutangazwa kupitia Gazeti la Serikali GN No. 725/2022”
Shahidi Kahaya alieleza historia yake ya kitaaluma kwa kina, akitaja elimu aliyoipata ndani na nje ya nchi, ikiwemo mafunzo ya “Forensic Video Examination” nchini Afrika Kusini, na “CCTV Forensic” nchini India mwaka 2024.
Aidha, alieleza kuwa amekuwa akifanya kazi katika uchunguzi wa video kwa zaidi ya miaka 12, ambapo jukumu lake kubwa ni kuchunguza uhalisia wa picha, video, na vielelezo vya kidigitali vinavyotumika katika kesi za jinai.
-Maelezo ya Kina Kuhusu Uchunguzi wa Kitaalamu-
Shahidi Kahaya alieleza kwa undani jinsi maabara yao inavyofanya kazi, akibainisha kuwa kila kielelezo kinapokelewa kwa barua rasmi na kusajiliwa katika Laboratory Book Register kabla ya kufanyiwa uchunguzi.
Alifafanua kuwa uchunguzi wa picha mjongeo (video) unafanyika kwa hatua tatu kuu: Mosi ni ukaguzi wa awali, pili uchunguzi wa kisayansi, na tatu uchambuzi wa kina.
Akieleza kwa lugha nyepesi, alisema:“Tunafanya uchunguzi wa awali kwa kutazama mwanga, rangi, na mwendelezo wa matamshi (lip movement) katika video. Tukiona kumeingiliwa au ‘jump cut’, tunajua kuna sehemu imehaririwa.”
Aliendelea kueleza kuhusu Meta Data Analysis akifafanua kuwa ni uchunguzi wa taarifa za ndani za kidigitali zinazopatikana ndani ya video au picha.
“Meta data ni taarifa kuhusu taarifa. Ndani ya video kuna data nyingine zinazotuambia chanzo, ukubwa, muda, na vifaa vilivyotumika kurekodi. Tunazitumia kugundua kama video imebadilishwa,” alisema.
Aidha, shahidi alieleza jinsi wanavyofanya “Cron Analysis” kwa lengo la kubaini iwapo video imepachikwa sauti au picha bandia kwa kutumia teknolojia ya “Artificial Intelligence (AI)” maarufu kama Deep Fake”
Kwa mujibu wa ushahidi wake, uchunguzi wa video unaohusiana na kesi ya Lissu ulifanyika baada ya kupokea barua mbili za maombi kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambazo zilikuwa na vielelezo vya “flash disk” na “memory card” zilizopewa alama maalum za maabara.
Baada ya uchunguzi, alisema, taarifa yake ya kitaalamu ilieleza kuwa vielelezo vilikidhi matakwa ya uchunguzi wa kisayansi.
Kesi hiyo ambayo inaendeshwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastun Ndunguru imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 16, saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa shahidi wa tatu ambapo upande wa Jamhuri utaendelea kumuhoji kabla ya Lissu kumuhoji maswali ya dodoso.