Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepanga kuanza kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Tundu Lissu, tarehe 12 Septemba 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili Gaston Shundo Garubindi, ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, hatua hiyo inalenga kusoma hoja za awali za kesi hiyo.
“Kesi hiyo itaanza kwa kusikilizwa hoja za awali kama ilivyopangwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam,” alisema Wakili Garubindi kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Ikumbukwe Agosti 18, 2025, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilibainisha kuwa kesi hiyo inakwenda Mahakama Kuu baada ya hatua za Kisheria kukamilika.
Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma mnamo Aprili 9,2025 muda mfupi mara baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara na kufikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Aprili 10,2025 mbapo alisomewa mashtaka ya uhaini pamoja na uchochezi.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania kosa la Uhaini ni kosa lisilo na dhamana na iwapo mshtakiwa akikutwa na hatia atakabiliana na adhabu ya kifo.
Hata hivyo mashtaka haya kwa Tundu Lissu yametafsiriwa kama ya kisiasa kutokana na kauli zake kinzani dhidi ya serikali.